Haruna: Nimekuja KMC kufanya kazi

NA MWANDISHI WETU

BAADA ya kutua katika klabu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC), kocha mpya wa timu hiyo, Harerimana Haruna, amesema amekuja kufanya kazi na kama ilivyo makocha wengi duniani, mafanikio ndiyo malengo makuu.

Akizungumza na BINGWA jana, mara baada ya kutambulishwa na Mwenyekiti wa Bodi wa timu hiyo, Bwenjamini Sita, Haruna alisema anahitaji wachezaji ambao wanajituma na wenye malengo ya kuleta mafanikio kwa timu na vile vile katika kipaji chake.

“Nimekuja kufanya kazi yenye mafanikio, hivyo naomba wachezaji tushirikiane katika kuleta matokeo chanya ya timu na kumaliza ligi katika nafasi nzuri.

“Nimefurahi kupata uongozi ambao unajali maslahi ya wachezaji na watendaji wa timu,” alisema Harerimana.

Kocha huyo atanatarajiwa kuwapo kwenye benchi la timu hiyo kwa mara ya kwanza itakapocheza na Mtibwa Sugar, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Awali akitambulishwa kocha huyo, Sita alisema  klabu hiyo umeingia mkataba wa mwaka mmoja na nusu  na Haruna, baada ya kukidhi vigezo walivyoweka.

Sita alisema Harerimana anachukua nafasi ya kocha Jackson Mayanja raia wa Uganda ambaye mkataba wake ulisitishwa kutokana na  timu kutokuwa na mwenendo mzuri Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Kimataifa.

Alisema Haruna amepitishwa na Bodi ya timu ambayo ilipitia maombi mengi ya makocha wa ndani na wa kigeni.

Sita alisema zoezi la kutafuta kocha halikuwa rahisi kutokana na ujuzi na uzoefu wa makocha waliomba kuchukua nafasi ya Mayanja na baada ya kuondoka, nafasi hiyo ilikuwa chini ya kaimu kocha mkuu, Hamadi Ally.

Alisema uongozi wa KMC unaimani kubwa na Haruna ambaye awali alikuwa anaifundisha timu ya Lipuli ya Iringa.

“Ni kocha ambaye amekidhi vigezo vyote ambavyo tumeweka na uongozi kuamua kuingia naye mkataba.  Kupitia yeye, tunaamini timu itafanya vyema na kurejesha ubora wake wa msimu  uliopita,” alisema Sitta.

Katika hatua nyingine, Uongozi wa timu hiyo umefikia makubaliano ya  kusitisha mikataba na wachezaji watano kutokana na sababu mbalimbali.

Wachezaji hao ni Aaron Lulambo, George Sangija, Rehani Kibingu, Melly Mongolare na Janvier Besala Bokongu na Vitalis Mayanga ameuzwa katika klabu ya Ndanda  ya  mkoani Mtwara.

 @@@@


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*