googleAds

Harambee Stars kuifuata DRC Madrid

PARIS, Ufaransa 

TIMU ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, inajiandaa kuondoka Paris, Ufaransa kuelekea Madrid nchini Hispania kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Jamhuru ya Kidemokrasia ya Congo ikiwa ni sehemu ya maandalizi kabla ya kuanza AFCON. 

Hii itakua ni mechi ya pili kwa Harambee Stars baada ya Ijumaa iliyopita kuifunga Madagascar bao 1-0 lililofungwa kipindi cha pili na nahodha Victor Wanyama kwa mkwaju wa penalti baada ya kipa Patrick Matasi kupangua penalti ya Madagascar kipindi cha kwanza. 

Baada ya ushindi huo, kocha mkuu Sebastian Migne alieleza kuridhika na kiwango kilichoonyeshwa na Harambee Stars ambao kwenye michuano ya AFCON wapo Kundi C pamoja na Taifa Stars ya Tanzania, Senegal na Algeria. 

“Ilikuwa bahati tulibadilika na kuja kivyingine kipindi cha pili na uzuri ni kwamba katika mchezo wa soka kuna nusu mbili. Tulikuwa na baadhi ya matatizo kipindi cha kwanza. Kwanza ni hali ya hewa na pili ni idadi kubwa ya wachezaji wapya ambao walichukua muda kuelewana.

“Ni mara yangu ya kwanza kuwaita Ayub Timbe na John Avire ambaye pia alikuwa anaichezea Harambee Stars kwa mara ya kwanza. Wawili hawa hawajawahi kucheza na wenzao katika timu na nina furaha tuliweza kubadilisha kila kitu kipindi cha pili,” alisema Migne.

Kocha huyo raia wa Ufaransa aliongeza kuwa ushindi huo (dhidi ya Madagascar) umewafanya wachezaji kujiamini kabla ya AFCON kuanza.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*