Hapa ndipo Liver ilipoishika Bayern

MUNICH, Ujerumani

 USIKU wa kuamkia jana ulikuwa ni wa furaha tena kwa mashabiki nchini England, hususan wa Liverpool, baada ya timu yao kuitupa nje Bayern Munich katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ilipoibugiza mabao 3-1 ikiwa ugenini katika Uwanja wa Allianz Arena katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 bora.

Wageni hao walionesha kiwango cha hali ya juu na hivyo kufanikiwa kuungana na timu za Ajax, Tottenham, Manchester United, Manchester City, FC Porto,  Barcelona na Juventus katika hatua ya robo fainali.

Katika mchezo huo alikuwa ni staa, Sadio Mane, ambaye msimu huu unaonekana kuwa  mzuri kwake katika kucheka na nyavu na ndiye aliyeipatia  Liverpool bao la kuongoza kwa shuti kali la guu lake la kushoto lililomshinda mlinda mlango wa Bayern, Manuel Neuer.

Hata hivyo, bao la kujifunga lililopatikana dakika ya 39 kwa kukwamishwa kimiani na beki wa kati wa Liver, Joel Matip, likayafanya matokeo kuwa sare hadi timu hizo zinakwenda mapumziko.

 Kipindi cha pili wageni walikuja kivingine na kulikuwa na hekaheka kila dakika ya mchezo.

Hata hivyo, beki wa Liver, Virgil Van Dijk, aliipatia tena bao la kuongoza timu yake ikiwa ni dakika 69 na huku  Bayern Munich wakizidi kubanwa kila sehemu ili wasiweze kuleta madhara kwa upande wa kikosi hicho cha Merseysiders.

Baada ya vuta nikuvute, Mane, aliweza kumaliza biashara kwa kuipatia bao la tatu timu yake ambalo liliwahakikishia tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kiwango hicho ni moja kati ya vikubwa kuoneshwa na Liverpool wakiwa ugenini katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuna sababu tatu ambazo ziliwasaidia kufikia mafanikio hayo.

 3. Ukuta imara ukiongozwa na Virgil Van Dijk

Hiyo ilikuwa ni siku nyingine nzuri katika safu ya ulinzi ya Liver ikiwa chini ya beki wao mahiri duniani, Virgil Van Dijk.

Beki huyo Mholanzi alitumia uwezo wake binafsi kumdhibiti straika tishio wa Bayern, Robert Lewandowski na wenzake akisaidiwa vyema na mwenzake, Joel Matip.

Licha ya bao la kujifunga la Matip, ukuta wa Reds ulikuwa imara kuzuia mashambulizi yote na baadaye, Van Dijk, akafuta makosa yaliyofanywa na mwenzake kwa kuipatia Liver bao la kuongoza kipindi cha pili cha mtanange huo.

 2.Mabadiliko ya Fabinho kufanya kazi

Liverpool walilazimika kufanya mabadiliko ya mapema baada ya nyota wao, Jordan Hendersongot, kuumia na nafasi yake ikachukuliwa na Fabinho.

 Mabadiliko haya ya mapema yanaonekana kuwa msaada mkubwa kwa  Liverpool kutokana na Fabinho kucheza kwa kiwango cha hali ya juu na huku akitibua mipira mingi ya Bayern katika safu ya kiungo.

Kipindi cha pili ilishuhudiwa akiweza kumtibulia nyota wa Bayern, Kingsley Coman, ambaye alikuwa akielekea langoni kwao.

Kiwango hicho cha Reds kipindi cha pili kiliwafanya waonekane kujiamini na huku wakitaka kuzitumia vyema dakika  45 zilizokuwa zimebaki.

  Katika kipindi hicho ilishuhudiwa vijana hao wa Klopp, wakipiga mashuti mengi, wakimiliki mpira na huku ulinzi kwa upande wao ukionekana kuwa ni wa hali ya juu jambo ambalo liliwafanya wastahili kushinda mechi hiyo.

  1. Kiwango cha hali ya juu cha  Sadio na kutokuwa na masihara langoni

Msimu huu ni mzuri mno kwa Sadio Mane, katika kupachika mabao tangu aanze kusakata kandanda.

  Raia huyo wa Senegal ndiye aliyeifanya  Reds iongoze kwa kupachika kwa shuti kali la mguu wake wa kulia.

 Mbali na kupachika bao hilo muda wote wa mchezo staa huyo alikuwa mwiba mkali kwa upande wa safu ya ulinzi ya  Bayern Munich, akisaidiwa na wenzake Roberto Firmino na Mohamed Salah.

Kiwango cha staa huyo kimekuja katika muda mwafaka kwa Liverpool na anaweza kuendelea kuisaidia Reds katika mechi zilizobaki msimu huu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*