googleAds

HAPA NDIPO CONTE ATAKAPOUMIA MSIMU UJAO

LONDON, England

CHELSEA wataweza kulitetea taji lao la Ligi Kuu England? Ndilo swali linalowaumiza vichwa mashabiki wa soka kuelekea msimu ujao unaotarajiwa kuanza keshokutwa.

 Msimu uliopita wakiwa chini ya Muitalia, Antonio Conte, wababe hao wa Magharibi mwa London, walikuwa moto wa kuotea mbali, wakichukua ubingwa kwa tofauti ya pointi saba.

 Lakini pia, ikiongozwa na kocha huyo aliyeshinda vikombe vitatu vya Serie A akiwa na Juventus, Chelsea iliweza kuwa timu ya kwanza kushinda mechi 30 katika msimu mmoja wa Ligi Kuu.

Hata hivyo, kuna sababu zinazoweza kumweka pabaya Conte katika safari yake ya kulichukua kwa mara ya pili taji la Ligi Kuu England.

Juzi, mchambuzi wa soka wa Sky Sports, ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, amedai kuwa haitashangaza kumuona Conte akitimuliwa Chelsea msimu ujao.

Tangu bilionea wa Urusi, Roman Abramovich, alipoinunua timu hiyo mwaka 2003, ameshawatimua makocha maarufu kwenye ulimwengu wa soka akiwamo Jose Mourinho aliyefukuzwa mara mbili, Carlo Ancelotti, Luiz Felipe Scolari na Claudio Ranieri, ambaye hakumaliza hata miaka miwili akiwa mkuu wa benchi la ufundi Stamford Bridge.

Hivyo, Carragher haoni kama Abramovich na mkurugenzi wake wa ufundi, Michael Emenalo, watamwonea aibu Conte endapo Chelsea itafanya vibaya msimu ujao.

Wengi wanaamini kuwa Chelsea hawataweza kufanya kile walichokifanya msimu uliopita na badala yake inaweza kuwa zamu ya vigogo wengine.

Rekodi ya Ligi Kuu England

Historia ya Ligi Kuu hiyo inaonyesha kuwa si rahisi kwa timu kutetea ubingwa. Katika misimu nane iliyopita, hakuna timu iliyoweza kuchukua taji hilo mara mbili.

Jose Mourinho alipojaribu kuibadili historia hiyo, yaani kutetea ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na Chelsea, aliishia kutimuliwa baada ya matokeo mabovu.

Aliishia kukorofishana mara kwa mara na wachezaji wake ambapo aliweza hata kumtaja Eden Hazard kuwa alikuwa akicheza chini ya kiwango.

Kuondoka kwa silaha zake

Huenda msimu ujao ukawa mgumu kwa Chelsea hasa baada ya kikosi hicho kupoteza baadhi ya wachezaji wake muhimu. Diego Costa, ambaye msimu uliopita alifunga mabao 20 haonekani kuwa kwenye mipango ya Conte na huenda akatimka.

Nafasi yake imeshachukuliwa na straika wa kimataifa wa Hispania, Alvaro Morata, mchezaji wa bei ghali ambaye hata hivyo hajawahi kufunga zaidi ya mabao 15 katika msimu mmoja.

Safu ya kiungo ya Blues pia imeondokewa na Nemanja Matic. Mserbia huyo alikuwa silaha muhimu kwa Conte msimu uliopita lakini msimu ujao atakuwa Old Trafford na Mourinho.

Kuziba pengo lake, Conte amemsajili Tiemoue Bakayoko kutoka Monaco.  Conte amewafungulia mlango viungo Ruben Loftus-Cheek na Nathaniel Chalobah.

Lakini pia, huenda ikachukua muda kumuona Antonio Rudiger aliyetokea Roma akiweza kuvaa viatu vya mkongwe na nahodha, John Terry.

Kuthibitisha kuwa bado Chelsea haijaimarika licha ya usajili wake, hivi karibuni, kocha Conte aliwaambia waandishi wa habari: “Soko la usajili bado liko wazi, hakika tunahaha kuboresha kikosi na ubora wa wachezaji.”

Ligi ya Mabingwa Ulaya

Msimu ujao, Conte atakuwa na kibarua kweli, ikizingatiwa kuwa mbali na Ligi Kuu, atakuwa akishiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya. Atalazimika kugawa nguvu kutokana na ugumu wa mashindano hayo.

Kurejea Ligi ya Mabingwa kutailazimisha Chelsea kuwa na kikosi kikubwa ili kumudu mshikemshike wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu.

“Kwa sasa tunapaswa kuboresha kikosi chetu kwa sababu tuna mechi nyingi na tunahitaji timu imara ya kushindana katika michuano hiyo,” alisema kocha Conte.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*