Hakikisha unayasahau haya uingiapo katika ndoa

KUOA ama kuolewa ni dalili ya mapenzi ya kweli. Ndiyo, wapo watu wanaingia kwenye ndoa bila kupendana, hiyo ni kesi nyingine.

Ila uhalisia ni kwamba watu wanaopendana na kuhitajiana kwa dhati katika maisha yao, wanatakiwa kuyaonesha hayo kwa kufunga ndoa.

Ukifunga ndoa maana yake unakubali kwa namna yoyote kwamba fulani ni mtu muhimu kwako na utakuwa mwaminifu na kumpa thamani stahili katika maisha yako.

Na kwa uamuzi huo, unakuwa umeweka bayana kwa walimwengu kwamba uliye naye ndiye sahihi sana kwa namna nyingi kuliko wengine. Huo ni ukweli halisi.

Ila pamoja na ukweli huu usio na shaka, maisha ya ndoa ni changamoto sana. Bila kuwa makini na changamoto hizo, unaweza kujikuta siku chache baada ya kula hicho kiapo unatamani kutoka nje ya ndoa.

Wapo wengi waliooa na kuolewa mwezi mmoja na kuachika mwezi uliofuata. Wapo waliotamani sana kuoa ila baada ya kuolewa wakajikuta wakijutia uamuzi wao. Sababu ni nini?

Sababu ziko nyingi, ila miongoni mwazo ni pamoja na watu kuingia katika ndoa na kutokuwa tayari kuishi kama wanandoa.

Mtu akiingia katika ndoa, anapaswa kufahamu kwamba badala ya kujifikiria yeye, inabidi pia afikiri kwa niaba ya mwenzake.

Mathalani, kama zamani alikuwa akienda club za usiku na marafiki na kurudi alfajiri, anapaswa kutambua sasa haiwezekani kufanya hivyo.

Baada ya kuingia katika ndoa, kila mmoja anapaswa kutambua kuwa ni ngumu kuishi katika ndoa kuliko kuifunga. Kwa maana hiyo anapaswa ajue anatakiwa kuwa mjanja, makini na mwenye kupima sana mambo kuliko alivyowahi kuwa kabla ya kuingia katika ndoa.

Ndoa inahusisha watu wawili. Watu wenye utashi tofauti, mitazamo tofauti na tafsiri ya mambo tofauti. Watu wa namna hii wakiacha kuwa makini basi kila siku katika maisha yao kutakuwa na ugomvi na hatimaye kujikuta wakiachana.

Katika ndoa hakuna mtu anayetakiwa kujiona yuko sahihi kwa kila kitu.  Katika ndoa kila mtu anatakiwa kujiona ana haki ya kuongea na wajibu wa kusikiliza.

Kila mtu katika nyumba akijiona anajua sana na ni makini sana kuliko mwenzie si tu atamfanya mwenzake akose amani, raha na furaha, ila pia atasababisha mahusiano yao yafubae na hatimaye yavunjike.

 Ili maisha ya ndoa yawe na furaha, kila mmoja anatakiwa awe na tafsiri chanya kwa mwenzake. Kama ukimuona mwenzako ni mkoseaji sana, malaya sana, hajui sana, basi utamfanya akuone unamnyanyasa na kumuona kituko, kitu ambacho hawezi daima kukivumilia.

 Kila binadamu anataka kujiona akiwa wa thamani, hadhi na heshima. Sasa ukimkosoa na kumkaripia ovyo ni kwa namna gani atajiona ana hadhi na heshima kwako?

Ukiwa ndani ya maisha ya ndoa, mbali na mambo mengine, ila tambua una jukumu la kuvumilia kama unavyopenda kuvumiliwa.

Haiwezekani mwenzako afanye kila kitu unachopenda. Na pia haiwezekani kwamba utamfurahisha kwa kila kitu katika maisha yenu yote.

Kwa sababu hiyo haiwezekani, basi ni busara sana kuvumiliana, kusikilizana na kukosoana kwa staha na heshima.

Binadamu huwa msikivu sana akiona anakosolewa kwa heshima, adabu na umakini. Ila huwa mkali, kiburi na mwenye chuki akiona anakosolewa kwa dharau.

Kila mtu akiona mtu fulani anamdharau basi na yeye huamua kumdharau. Sasa ndoa yenu itakuwa na furaha vipi ikiwa kila mmoja anamdharau mwenzake?

Mnapojikuta mko katika mgogoro katika ndoa, epuka kutafuta ushindi, ila kwanza tafuta njia bora ya kutatua mgogoro huo. Mwenzako akiwa anasema mpe nafasi, mwache aelezee hisia zake, mwache ateme sumu yote.

Mtu mwenye hasira anapoongea anapunguza kiwango cha hasira zake. Usimzuie kuongea.

 Ukimzuia si tu utakuwa unachochea hasira zake, ila pia ndiyo itakuwa tiketi ya kuingia katika ugomvi mkubwa zaidi kati yenu. Kumbuka ndoa ni busara na hekima.

 ramadhanimasenga@yahoo.com

instagram: g.masenga


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*