Guardiola: Siwezi kumpiku Hodgson

 LONDON, England

KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola, amesema kwamba anavyoamini hawezi kumpiku mwenzake wa  Crystal Palace, Roy Hodgson na kuendelea kubaki kwenye soka hadi kufikia umri wa miaka  71.

Jana Hodgson na timu yake ya Palace walikuwa wakiwakaribisha vijana wa Guardiola masaa mawili kabla ya vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool kuikaribisha Chelsea katika Uwanja wa Anfield.

Mbio za kuwania ubingwa msimu huu bado zinaendelea kushika kasi na mabingwa hao watetezi watashuka katika uwanja wa  Selhurst Park kwa tahadhari, kwani waliwahi kuambulia kipigo cha mabao 3-2  kutoka kwa timu hiyo wakati wa sikukuu ya Krismasi.

Kwa sasa Hodgson ndiye kocha mwenye umri mkubwa kufundisha timu za Ligi Kuu England na Guardiola anasema kwamba hana ndoto za kumfikia kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya England.

“Kwa upande wangu haiwezekani, kwa sababu inahitaji moyo,” kocha huyo mwenye umri wa miaka 48 aliuambia mkutano wa waandishi wa habari juzi.

 “Ni vizuri sana kukutana naye kesho (jana). Ninafikiria kufanya kitu kingine kabla sijafa. Japokuwa naipenda kazi yangu, lakini mara zote huwa nafikiria kufanya kitu kingine tofauti. Kuna mke  na familia yangu, ila kufikisha miaka 71 katika soka haiwezekani,” aliongeza kocha huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*