GUARDIOLA: NYIE HANGAIKENI TU, NITAWANYOOSHA

MANCHESTER, England


WAKATI timu pinzani zilizoshindwa kuizuia vema Manchester City isichukue ubingwa msimu uliopita zikiwa zimejiandaa vilivyo kuwapa upinzani, kocha wa timu hiyo, Pep Guardiola, ametoa onyo kali akisema msimu huu amejiimarisha zaidi.

Man City walivunja rekodi za Ligi Kuu England msimu uliopita ambao waliumaliza na pointi 100, wakiwaacha wapinzani wao wa jadi, Manchester United kwa tofauti ya pointi 19.

Kuelekea ufunguzi wa ligi hiyo usiku wa leo na kuendelea wikiendi hii, vijana hao wa Guardiola wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kwa mara nyingine.

Na Guardiola anaamini kuwa kikosi chake kitashangaza zaidi msimu huu, akiwa na matumaini kwamba nyota wake kama Sergio Aguero, Kevin De Bruyne na David Silva, watauwasha moto ipasavyo.

“Unajua kila mchezaji ana nafasi ya kujiimarisha mwenyewe kila siku. Kama leo atapiga shuti kwa mguu wa kulia, kesho atautumia vizuri ule wa kushoto,” alisema Guardiola.

“Iwapo utahitaji kuimarisha uwezo wa wachezaji basi ni timu nzima inaimarika. Kila wakati ni wa kuboresha.”

Hata hivyo, Guardiola aliongeza kwamba, hategemei mwaka huu kuwa mwepesi kwa timu yake kutetea ubingwa kutokana na jinsi wapinzani wake walivyojipanga.

“Tulichokifanya sisi timu yoyote inaweza kukifanya, hasa kwa zile tano kubwa,” aliongeza.

“Ningependa pia kusema zote zina uwezo, Manchester United, Chelsea, Arsenal, Tottenham, Liverpool, wote hao wataleta upinzani.”


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*