googleAds

Goodluck Gozbert: Sijawahi kujua kujitofautisha sababu Mungu ndiye mtoaji

KARIBU msomaji wa safu hii ya Jiachie na Staa Wako inayokupa nafasi ya kuwa karibu na watu maarufu uwapendao. Leo tupo na Goodluck Gozbert, mwimbaji makini wa Injili ambaye huduma yake imefanikiwa na sasa anatamba na wimbo mpya Nibadilishe.

SWALI: Teddy Joseph wa Kogongwa Kahama anauliza kwanini uliamua kutumia majina mawili ya Goodluck Gozbert na  Lollipop kama mtunzi na produza?

Goodluck:  Hakuwahi kuwa ndoto yangu kuwa mtunzi wa nyimbo na mtayarishaji wa muziki ila ni mapito tu, unafika wakati unakosa ada harafu nipo mtaani, kazi hakuna lakini Mungu amenibariki kipaji, nikaanza kutembea studio nyingi nikawa sipati nafasi.

Nikapata studio moja wakakubali kile nilichokuwa nafanya, nikaanza kwa kupiga kinanda, nikawa natumiwa nauli, baadaye nikawa nanunuliwa chakula, baadaye nikaanza kupewa shilingi 50,000, baadaye nikawa napewa nusu ya pesa inayolipwa studio, baadaye nikawa napaga nilipwe kiasi gani kisha nikafungua studio yangu mwenyewe.

SWALI: Reynald Misango wa Ruangwa Lindi anauliza mwaka jana ulipata mwaliko Ikulu, je ni vitu gani ambavyo Rais Magufuli alikwambia na hauwezi kusahau na ilikuongezea nini kwenye muziki wako?

Goodluck: Sikuwahi kujua kama anafuatilia kazi zangu pia sikuwahi kuota kama kuna siku Rais wa nchi niliyozaliwa anaweza kuwa shabiki wa wimbo wangu, kwahiyo ile tu kuniambia ninafanya kazi nzuri, endelea songa mbele ilikuwa kitu kikubwa sana kwenye maisha yangu hata nikiwa na watoto kesho nitawaambia.

Kuna heshima fulani ilikuja kwangu, kwenye ukoo wangu, kwa familia yangu na kwenye huduma yangu kiufupi ilikuwa njema kwaajili ya utukufu wa Mungu pia kulikuwa na mabadiliko makubwa sana japo yalikuja na ‘negative impact’ (athari hasi) maana kuanzia pale hakuna mtu anaamini kama Goodluck naweza kuwa na matatizo kiuchumi.

SWALI: Dullah Mpotwile wa Tegeta Dar es Salaam anauliza tumtambue Goodluck Gozbert kama nani mtunzi, mwimbaji au prodyuza na ilikuwaje ukaingia kwenye muziki?

Goodluck: Mimi ni kijana wa Kikristo niliyempa Yesu maisha yangu na niliyeamua kutumika kwaaajili ya ufalme wa Mungu. Ni historia ndefu lakini kwa ufupi nilikuta mama na dada zangu wanaimba kwaya.

Nikafanikiwa kuwa mwimba kwaya, nikaingia kwenye masuala ya kutayarisha muziki, wakati najifunza kutayarishaji muziki nikawa natayarisha kazi zangu mwenyewe ambazo zilipoanza kutoka zikafanya vizuri.

SWALI: Pidi Japhet WA Bukoba anauliza unajitofautisha vipi na waimbaji wenzio?

Goodluck: Sijawahi kujua kujitofautisha, unajua kwenye kanisa kuna huduma tofauti tofauti, kuna  wachungaji, walimu, wainjilisti na kila mmoja ameitwa kwa nafasi yake kwa sehemu yake huwezi kujitofautisha sababu Mungu ndiyo anayetoa, vile ulivyoumbwa ndiyo ndiyo tofauti yako na mtu mwingine.

SWALI: Dennis Nestory kutoka Biharamulo anataka kujua mama yako ambaye amekupambania sana ana nufaika vipi na mafanikio yako?

Goodluck: Sioni kama amenufaika hata kidogo na muziki wangu ila amenufaika kwamba ana mtoto ambaye anamjua Kristo, hicho tu ni kikubwa sababu najua vijana wengi wamepotea.

Kuna vijana wanaishi maisha ya dawa za kulevya, watu wamepinda mtaani lakini akiniangalia anasema afadhali mwanangu naamini mimi nilikuwa nimepinda ila nilipookoka nikabadilika, iwe nimemjengea nyumba, nimemnunulia gari bado havitatosha kusema mama amenufaika kupitia muziki wangu.

SWALI: Castro James wa Tarime Mara anauliza kwanini kwenye wimbo wako umecheza mtindo wa Shaku Shaku ambao unatumika na wasanii wa Bongo Fleva?

Goodluck: Mtoto anajifunza kile anachokiona, naomba niseme na wale walokole wenzangu tunatofautiana sana mimi ndiyo kwanza naanza nahitaji kujifunza, nilipokuwa nakua sikuwa nacheza staili kwa kufikirika nilikuwa nacheza michezo yote ambayo naiona watu wengine wanacheza na kilichonivutia nilikitumia na ambacho hakikunivutia sikukitumia.

Watu wote hata walokole wasijifanye hawajui ‘twerking’, wanajua ku ‘twerk’ ni nini lakini hawakukuta kuna binti ame ‘twerk’ kwenye video ya Nibadilishe sababu binafsi sipendezwi na ile staili, naona kama ni tangazo la kitu ambacho siyo poa kwa kanisa, kwahiyo shaku ni inaweza kuwa staili ngumu kidogo lakini mtaizoea kama mlivyozoea kiduku.

Wiki ijayo tutakuwa wachekeshaji Tin White au Ringo tuma maswali yako kupitia namba hapo juu, meseji tu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*