Gigy Money ajiweka mbali na bifu

NA KYALAA SEHEYE

MSANII wa Bongo Fleva, Zawadi Stanford ‘Gigy Money’, amesema hataki kujiingiza katika uhasama wowote katika muziki kwa sababu ana njaa na hajui nani atakayemsaidia atakapokuwa na shida.

Gigy ameliambia Papaso la Burudani kuwa, anapenda muziki mzuri na anashirikiana na wasanii wote hapa nchini, hivyo anaomba asihusishwe na uhasama wowote katika tasnia.

“Mimi nina njaa zangu, hivyo siwezi kuwa na timu, hasa kwa wasanii wenzangu, kwanza sijui nani atakuja kuniokoa pindi nitakapopata matatizo, mimi ni masikini, sijui mwisho wangu utakuwaje,” alisema Gigy Money.

Aidha, Gigy Money leo anatarajia kuungana na wasanii kama Diamond Platnumz, Linah, Rayvanny, Harmonize, Lavalava, Mbosso, Queen Darleen, Dudubaya, Chin Bees, Juma Nature, Country Boy, Moni, Young Killer, Nikki Mbishi, One The Incredible, Stereo,  Khadija Kopa, Ice Boy na Dully Sykes, kutumbuiza katika tamasha la Wasafi litakalofanyika uwanja wa Samora, Iringa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*