Gattuso awapa neno mastaa AC Milan

MILAN, Italia

KOCHA Gennaro Gattuso amewapa neno mastaa wake, AC Milan akiwataka kuonesha hasira ya kurejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya juzi vinara hao wa Ligi ya  Serie A kurejea nne bora kutokana na ushindi wa mabao 3-0 walioupata dhidi ya Cagliari.

Mwishoni mwa wiki timu za Atalanta, Roma na Lazio zilishinda mechi zao na huku AC Milan wakishika nafasi ya saba kabla ya mechi yao hiyo iliyopigwa katika Uwanja wa San Siro.

Hata hivyo, bao alilojifunga nahodha wa  Cagliari, Luca Ceppitelli, Lucas Paqueta kafungua akaunti yake ya mabao kwenye klabu hiyo ya Rossoneri na kisha  Krzysztof Piatek akaendeleza moto wake ambao uliwapa pointi zote tatu.

Pointi hizo ndizo zilizoifanya AC Milan kuchupa hadi nafasi ya nne na Lazio ikishika ya saba na sasa kikosi hicho cha Gattuso kinajiandaa kuivaa Atalanta ambayo inashika nafasi ya tano Jumamosi ijayo.

Kutokana na hali hiyo, Gattuso anawataka vijana wake kuendeleza moto huo kipindi chote kilichobaki msimu huu ili waweze kumaliza ligi wakiwa nne bora na kufuzu kucheza michuano ya Ligi ya Mabigwa Ulaya.

“Tumefanya vizuri na tumecheza kandanda safi ambalo tungeweza kufunga mabao mengi,” kocha huyo aliiambia Sky Sport Italia.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*