Fei Toto arejesha raha Jangwani

*Yaichapa JKT Tanzania kimoja safi Mkwakwani, watimkia Moro kuiwinda Simba

*Mo Banka arejesha kampa kampa tena, sasa kazi ipo Jumamosi

NA ZAITUNI KIBWANA

YANGA imefanikiwa kuichapa JKT Tanzania bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, huku kiungo wa Wanajangwani hao, Mohammed Issa ‘Mo Banka’, aking’ara vilivyo katika mechi yake hiyo ya kwanza tangu amesajiliwa Jangwani.

Kwa matokeo hayo, Yanga imeendelea kukalia kiti cha uongozi wa ligi hiyo, ikifikisha pointi 58 kutokana na mechi 23, huku Azam iliyoshuka dimbani mara 21, ikifuatia ikiwa na pointi 48, wakati Simba wanaoshika nafasi ya tatu wakiweka kibindoni pointi 36 walizovuna ndani ya mechi 15.

JKT Tanzania kwa kupoteza mchezo wao huo wa 26, wamebaki katika nafasi yao ya saba wakiwa na pointi 32.

Alikuwa ni kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyeifungia timu yake bao pekee la ushindi katika mchezo huo, akizitikisa nyavu za JKT Tanzania dakika ya 26 kwa guu lake la kushoto, akiunganisha pasi murua kutoka kwa beki wa kushoto, Gadiel Michael.

JKT Tanzania ndio waliokuwa wa kwanza kulifikia lango la wapinzani wao ambapo dakika ya tisa, Ally Ahmed Shiboli, akiwa ndani ya eneo la hatari almanusura aipatie timu yake bao la kuongoza, lakini shuti lake lilipaa.

Ibrahim Ajib nusura aipatie Yanga bao dakika ya 36, lakini shuti lake liliokolewa na kipa wa JKT Tanzania, Patrick Muntary, ikiwa ni baada ya kupokea pasi ya Gadiel.

Dakika ya 48, George Mande aliikosesha JKT Tanzania bao baada ya kupiga shuti lililopaa baada ya kupokea pasi ya Dickson Chota.

JKT Tanzania walikosa bao dakika ya 78 baada ya Hassan Materema kupiga mpira wa kichwa ambao uliokolewa na kipa wa Yanga, Ramadhan Kabwili.

Pamoja na ushindi huo, Yanga jana walionyesha uhai kidogo wakicheza soka la kuvutia, huku wachezaji wakionekana kujituma mno japo uwanja haukuwa rafiki kutokana na kuwa na vipara vya hapa na pale.

Kwa upande wao, pamoja na kupoteza mchezo huo, JKT Tanzania walicheza vizuri, wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Yanga, lakini bahati haikuwa yao.

Baada ya mchezo huo, kikosi cha Yanga kiliunganisha safari ya kwenda Morogoro kuweka kambi ya kuwawinda watani wao wa jadi watakaocheza nao Jumamosi hii katika mchezo wa ligi hiyo, utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, ameliambia BINGWA jana kuwa kikosi chao kinatarajia kuondoka Tanga leo asubuhi kwenda Morogoro kuweka kambi ya muda kabla ya kurejea Dar es Salaam tayari kwa pambano hilo la watani la kukata na shoka.

JKT Tanzania: Patrick Muntary, Anuary Kilemile, Dickson Chota/Ally Bilal dk56, Frank Nchimbi, Mohamed Fakhi, George Mande, Mwinyi Kazimoto, Samweli Kamuntu/Said Uyaya dk76, Ally Ahmed Shiboli/Najim Magulu dk88, Edward Sonyo na Hassani Materema.

Yanga: Ramadhani Kambwili, Paulo Godfrey, Gadiel Michael, Andrew Vincent, Abdallah Haji, Faisal Salum, Mrisho Ngasa/Mohammed Issa ‘Mo Banka’ dk58, Papy Tshishimbi, Ibrahim Ajib/Deus Kaseka dk67, Amissi Tambwe na Pius Buswita/Kelvin Yondani dk76.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, wenyeji KMC walilazimishwa sare ya bao 1-1 na Alliance ya Mwanza.

Bao la KMC lilifungwa na Abdul Ilal dakika ya 50, huku Patrick Israel akiisawazishia Alliance dakika ya 64.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*