FEI TOTO AMFUNIKA TSHISHIMBI YANGA

NA MICHAEL MAURUS


KIUNGO mpya wa Yanga, Feisal Salim ‘Fei Toto’, ameonyesha kiwango cha hali ya juu katika suala zima la kupiga pasi murua, kukaba na kutawanya mipira hivyo kuwa na uwezekano wa kumng’oa Pappy Tshishimbi, nafasi ya kiungo mkabaji.

Fei Toto katika mazoezi ya Yanga yanayoendelea kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia mjini hapa, amekuwa mwepesi kuomba pasi na kugawa, lakini pia kupora mipira.

Kati ya mambo ambayo amekuwa akiwakuna mashabiki wanaojitokeza kufuatilia mazoezi hayo, ikiwamo mechi ya kirafiki waliyocheza juzi dhidi ya Morogoro Tanzanite Academy, ni uwezo wake wa kupiga pasi ndefu zinazowafikia walengwa kama alivyokuwa akifanya Athumani Idd ‘Chuji’ aliyewahi kuichezea timu hiyo.

Uwezo wake huo umemfanya kufananishwa na Chuji ambapo mashabiki wanaamini ndiye mbadala sahihi wa kiungo wao huyo wa zamani.

Lakini pia, wepesi wake wa kuwasogelea mabeki wake hasa wa pembeni wanapokuwa na mpira, umewakuna wengi kwani atawasaidia mno akina Juma Abdul, Gadiel Michael, Haji Mwinyi na wengineo kutopata shida kutafuta mtu wa kumpa pasi pindi wanapoanziwa na kipa.

Kwa kifupi, Fei Toto iwapo ataendelea na kiwango chake, ni mkombozi kwa mabeki wa pembeni, wa kati na hata washambuliaji.

Kutokana na uchezaji wa Mzanzibari huyo, ni wazi Tshishimbi atalazimika kupandishwa ‘dimba la juu’ yaani kiungo mshambuliaji, huku Fei Toto akiachiwa ‘dimba la chini’.

Hata hivyo, bado Fei Toto anatakiwa kukaza hasa kwani kuna Said Juma Makapu ambaye naye si wa kubeza akionekana kujituma mno mazoezini ili kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.

Uzuri wa Makapu, ana uwezo wa kucheza namba zote za nyuma, kuanzia mbili, nne, tano na sita hali ambayo inamhakikishia nafasi katika kikosi hicho chini ya Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera raia wa DR Congo.

Pia, yupo Maka Edward ambaye naye ameonyesha kupania kutinga kikosi cha kwanza kutokana na jinsi anavyopambana mazoezini, lakini pia katika mechi ya kirafiki ya juzi.

Kwa ujumla, wachezaji wote wa Yanga wameonekana kupambana vilivyo ili kuibeba timu yao msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakapoanza.

Yanga msimu uliopita iliporwa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na watani wao wa jadi, Simba na sasa wanajipanga kuona ni vipi wanamrejesha ‘mwali’ wao Jangwani.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*