googleAds

EYMAEL: YANGA NINAYOITAKA MTAIPENDA

Tima Sikilo

KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, amewataka Wanajangwani kuwa wapole kwani anahitaji kuipika timu yao kuanzia chini ili kuwa moto wa kuotea mbali.

Eymael amejiunga na Yanga katika kipindi cha dirisha dogo la usajili akichukua nafasi ya Mwinyi Zahera aliyetimuliwa.

Mpaka sasa kikosi hicho chini yake, kimeshacheza michezo minne, akishinda miwili na kupoteza miwili.

Akizungumza na BINGWA juzi, kocha huyo alisema katika timu jambo la muhimu ni kupata ushindi ambao lazima msingi wake uandaliwe kuanzia safu ya ulinzi hadi ya ushambuliaji.

“Pamoja na mtokeo tunayoyapata, lakini nahitaji kuanza kujenga msingi wa timu ili kila mchezaji aweze kufanya vizuri hali itakayoifanya timu kwa ujumla iwe nzuri.

“Wengi hupenda matokeo, lakini huwezi kujenga nyumba bila kuimarisha msingi, nikifanikiwa hilo, nitakuwa nimepata kikosi ambacho ninakihitaji kitakachokuwa kikipata matokeo mazuri kila mechi,” alisema.

Alisema tayari ameanza kazi hiyo mazoezini na ana imani majibu yataanza kupatikana muda si mrefu katika mechi zao kwa kutoa vipigo kwa kila timu watakayokutana nayo, lakini pia kutandaza soka maridadi.

Baada ya kuichapa Tanzania Prisons mabao 2-1 Jumapili iliyopita katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam, Yanga inatarajiwa kushuka dimbani tena mwishoni mwa wiki hii kuvaana na Mtibwa Sugar, ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*