EYMAEL, KAGERE WAPATA AHUENI

ZAINAB IDDY

KAULI ya Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, hususan kuhusu karantini itakua imepokelewa vyema na wachezaji na makocha wakigeni walio nje ya nchi. 

Miongoni mwa wachezaji walio nchini kwao tangu ligi kusimama Machi 17 mwaka huu ni Meddie Kagere (Rwanda), Francis Kahata (Kenya), Clatous Chama (Zambia) na Sharaf Shiboub (Sudan) huku makocha ni Luc Eymael (Ubelgiji) na Riedoh Berdien (Afrika Kusini). 

Tangu masharti ya kutotoka nje ‘lockdown’ yalegezwe nchini Ubelgiji na Rwanda, kocha wa Yanga, Eymael na straika wa Simba, Kagere wamekuwa wakionyesha nia yao ya kutaka kurudi nchini. 

Hata hivyo hilo likawa linashindikana kufuatia anga za nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania kufungwa ikiwa ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa kupambana na kusambaa ugonjwa wa virusi vya corona. 

Aidha kulikuwa na suala la kuingia karantini ya siku 14 kwa wageni wote wanaowasili nchini ambapo vipimo vya covid-19 vitachukuliwa. 

Eymael alionyesha nia yake ya kujitenga kwa siku 14 pindi atakapowasili nchini kabla ya kujiunga na kikosi chake tayari kwa michezo ya ligi iliyosalia. 

Machi 3 mwaka huu wakati Rais Magufuli alipokuwa anamuapisha Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Mwigulu Nchemba, Ikulu ya Chato mkoani Geita, alisema anafikiri kuruhusu Ligi Kuu Bara kuendelea. 

Ni tamko lililopokelewa vyema na wachezaji na makocha ambao walianza kuweka utaratibu wa mazoezi wakisubiri maelekezo zaidi kutoka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). 

Jana kwa mara nyingine tena, Rais Magufuli alieleza nia yake ya kuruhusu michezo iendele na kuongeza ametoa maagizo kwa Waziri wa Utalii na Maliasili pamoja na Waziri wa Uchukuzi kuruhusu ndege kutua na ameondoa karantini kwa wageni wanaowasili nchini ila akasisitiza wapimwe joto ya mwili. 

Rais Magufuli alisema hayo katika Kanisa la KKKT Usharika wa Chato mkoani Geita muda mchache baada ya kumalizika kwa ibada ya Jumapili iliyoongozwa na Mchungaji Thomas Kangeizi. 

Alisema idadi ya wagonjwa wa virusi vya corona katika vituo vilivyotengwa imepungua hivyo anaangalia wiki inayoanza leo kama hali itaendelea kuwa ya kuridhisha kama ilivyo hivi hivi, ataamua kufungua vyuo na kuruhusu michezo iendelee.

Rais Magufuli alisema michezo ni sehemu ya burudani kwa Watanzania hivyo lazima maisha yaendelee.

“Kwa hali hii, kama wiki tunayoianza kesho (leo) itaendelea hivi, nimepanga kufungua vyuo ili wanafunzi wetu waendelee kusoma, lakini nimepanga pia kuruhusu michezo iendelee kwa sababu michezo ni sehemu ya burudani, maisha lazima yaendelee,” alisema.

“Ugonjwa huu wa corona ni vita kama vita nyingine, wakati unaanza nilisema siwezi kuruhusu ‘lockdown’, unafungiwa ndani eti usitembee usiku kana kwamba corona inatembea usiku tu, nikasema hapana.”

Hatua ambayo Serikali ilichukua Machi 17 mwaka huu kufuatia mlipuko wa janga la virusi vya corona ilikuwa kufunga shule na vyuo vyote, na kusitisha shughuli zote za michezo. 

Serikali pia ikawataka wananchi kufuata maelekezo wanayopewa na Wizara ya Afya na kusisitia kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima. 

Kauli ya jana ya Rais Magufuli inazidi kutoa matumaini ya Ligi Kuu Bara kuendelea tena na sasa ni suala la kuhesabu muda lini TFF itatoa ratiba mpya na utaratibu utakaotumika mechi zilizobakia za ligi zichezwe na kumalizika 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*