googleAds

ETI ZIDANE ANA HASIRA YA KUBEBA MATAJI LUNDO 

SKOPJE, Macedonia

KWA lugha nyingine unaweza kusema kuwa huku sasa ni kutafuta sifa baada ya kocha wa timu ya Real Madrid kusema kwamba, yeye pamoja na timu yake wana hasira ya kuhakikisha wanabeba mataji mengi kadiri iwezekanavyo.

Zidane aliyasema hayo usiku wa kuamkia jana baada ya Real Madrid kunyakua ubingwa wa Kombe la Uefa Super Cup, kwa kuibugiza Manchester United kwa mabao 2-1 katika mchezo huo wa fainali uliopigwa katika Uwanja wa Philip II Arena uliopo mjini Skopje, nchini Macedonia.

Walikuwa ni wachezaji Casemiro na  Isco waliochana nyavu wakati  mabingwa hao wa  La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiibuka na ushindi huo dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi ya Europa.

Casemiro ndiye alikuwa wa kwanza kuziona nyavu ikiwa ni dakika ya 24 ya kipindi cha kwanza na Isco ambaye aliibuka shujaa wa mechi akaongeza la pili dakika ya saba ya kipindi cha pili, kabla ya Romelu Lukaku kupunguza moja ukiwa umebaki muda mchache  mtanange huo umalizike.

Taji hilo linakuwa ni la tatu kwa Real Madrid katika michuano hiyo ya Super Cup tangu mwaka 2014.

“Sote tunafahamu tuna hazina kubwa ya vipaji na kwa kuvitumia tunaweza kupata mafanikio makubwa,” alisema kocha mkuu huyo Zidane ambaye ameweka rekodi ya kuwa kocha wa nne kwa mafanikio katika timu hiyo.

“Tuna hasira kutokana na kwamba, mara zote huwa tunapenda kupata zaidi na zaidi,” aliongeza.

Akizungumzia kuhusu msimu mpya wa ligi ya La Liga, Zidane ambaye mchezo huo ulikuwa ni wa 66 katika mashindano yote, alisema wanachokifahamu kila mechi itakuwa ni ngumu kwao na wapinzani wao watakuwa wakitoa upinzani mkubwa msimu mzima na akasema kuwa jambo hilo wanatarajia kuanza nalo Jumapili ijayo


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*