googleAds

ETI NINI… Liverpool yashikilia kibarua cha Solskjaer, watabiri atafukuzwa kama Mourinho

MANCHESTER, England

HALI inazidi kuwa mbaya ndani ya kikosi cha Manchester United ambayo inafundishwa na Ole Gunnar Solskjaer aliyechukua mikoba ya Jose Mourinho, Desemba mwaka jana.

Tayari Manchester United wapo nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu England, baada ya michezo nane kuchezwa ambayo wameshinda miwili, kufungwa mitatu na kutoa sare mara tatu.

Ni matokeo mabaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya klabu hiyo huku Solskjaer akiwa na wastani wa asilimia 48 za ushindi ndani ya kikosi hicho. Wastani mdogo zaidi kwa makocha tangu Sir Alex Ferguson aondoke Manchester United.

Lakini taarifa kutoka nchini England zimebainisha kuwa Solskjaer atafukuzwa ndani ya klabu hiyo kama atafungwa mchezo ujao dhidi ya Liverpool utakaochezwa Oktoba 20, mwaka huu katika Uwanja wa Old Trafford.

Taarifa hizo zimevuja na kumfanya kocha huyo kuwa katika kiti moto kama ilivyokuwa kwa Jose Mourinho ambaye alifukuzwa hapo baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Liverpool katika Uwanja wa Anfield.

Liverpool ambao wanaongoza Ligi Kuu England kwa kushinda michezo yote nane na kujikusanyia pointi 24, wataenda Old Trafford ambako hawajawahi kupata ushindi tangu mwaka 2013 kuwakabili mahasimu wao.

Wachambuzi wa kituo cha ESPN wanaamini kama ilivyokuwa kwa Mourinho msimu uliopita, basi hali hiyo inaweza kumkuta Solskjaer ambaye anakinoa kikosi hicho cha mabingwa wa zamani wa England.

“Dalili zinaonyesha atafukuzwa kama akifungwa na Liverpool, sidhani kama mabosi wa Manchester United wataendelea matokeo mabaya ya kikosi chao.

“Hali inazidi kuwa mbaya, wachezaji sidhani kama wanamuelewa Solskjaer, hakuna anayeonyesha kiwango kizuri kama wakati ule alipoingia kwa mara ya kwanza akiwa kocha wa muda,” alisema mchambuzi mmoja.

Hata hivyo, Manchester United walitoa taarifa za kuendelea kumwamini kocha huyo, wakiamini hiki ni kipindi cha mpito cha kujenga kikosi chao kwa miaka ijayo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*