ESSIEN ATABIRI HAZARD KUBAKI CHELSEA

LONDON, England


 

KIUNGO wa zamani wa Chelsea,  Michael Essien, amesema ana matumaini kuwa staa wa timu hiyo, Eden Hazard,  ataendelea kukitumikia kikosi hicho na huku akiendelea kung’ara kwa kiwango chake.

Hazard alikuwa akitajwa kuondoka kwenye klabu hiyo ya  Stamford Bridge wakati wa kipindi cha usajili na kwenda kujiunga na  Real Madrid ambayo inasemekana kumhitaji, baada ya Julai kukiri kuwa anajaribu kwenda kutafuta kitu tofauti.

Hata hivyo, nyota huyo raia wa Ubelgiji, baadaye alisema anajisikia mwenye furaha kubaki na kujifunza zaidi chini ya kocha wake mpya, Maurizio Sarri na tayari msimu huu ameshafunga mabao  saba katika michezo nane aliyokwishacheza likiwamo la ushindi alilolifunga dhidi ya Liverpool katika michuano ya Kombe la EFL.

Hazard atakuwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake wakati dirisha kubwa la usajili mwakani litakapofunguliwa, lakini  Essien ambaye aliwahi kutwaa mataji nane akiwa na  Blues, hana wasiwasi kuhusu hatima ya staa huyo.

“Awali ya yote bado ni vizuri kwetu kuwa naye kama mchezaji mzuri,” staa huyo aliuambia mtandao wa  Omnisport. “Alikuwa na kiwango kizuri wakati wa fainali za Kombe la Dunia na aliporejea amekuwa akifanya vizuri mpaka sasa,” aliongeza staa huyo raia wa Ghana.

“Tuna matumaini ataendelea kuibeba timu mpaka mwishoni mwa msimu na ndipo tukapoona kitakachojitokeza,” aliongeza zaidi nyota huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*