googleAds

Dkt. Msolla aja na mkakati kabambe

MICHAEL MAURUS, MOROGORO MWENYEKITI wa Yanga, Dkt. Mshindo Msolla, amepanga kukutana na mchezaji mmoja mmoja ili kuwaweka sawa kabla ya kuanza kwa msimu ujao, wakikabiliwa na michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika. Akizungumza na BINGWA jana alipotembelea mazoezi ya timu hiyo ya asubuhi yaliyoambatana na mechi ya kirafiki dhidi ya Moro Kids, kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia, mjini hapa, Dkt. Msolla alisema kuwa kuna baadhi ya wachezaji wana uwezo mkubwa lakini wanashindwa kuutendea haki.

“Tanzania tuna wachezaji wazuri na wenye vipaji vya hali ya juu, lakini baadhi yao wanashindwa kuvitendea haki, sasa nadhani kuna umuhimu wa kuzungumza na mchezaji mmoja mmoja ili kuwaweka sawa,” alisema kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa, Taifa Stars. Alisema alitamani kufanya hivyo kati ya jana hadi kesho, lakini kutokana na jinsi alivyobanwa na ratiba, yakiwamo majukumu yake ya kikazi nje ya Yanga, imeshindikana, akipanga kutekeleza hilo atakapopata muda kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

Wakati huo huo, Dkt. Msolla jana alizungumza na wachezaji wa Yanga waliopo kambini mjini hapa, akiwataka kutekeleza majukumu yao ipasavyo, huku akiahidi uongozi wake kutimiza wajibu wao kadri itakavyowezekana. Kiongozi huyo aliyasema hayo katika ukumbi wa kambi ya Yanga, kwenye hoteli ya Kings Way, iliyopo Msamvu, mjini hapa. Katika hatua nyingine, Dkt. Msolla amezungumza na wanachama wa Yanga wa Morogoro na kuweka mikakati kabambe ya kuiwezesha kambi ya timu hiyo iliyopo mjini hapa kuwa ya mafanikio makubwa, lakini pia kiongozi huyo akiwataka Wanajangwani hao wa Mji Kasoro Bahari, kushirikiana bega kwa bega na uongozi wa juu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*