googleAds

DITTO:KUTOKA WATUPORI, LA FAMILIA HADI THT

 

NA GLORY MLAY

MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Lameck Ditto ‘Ditto’, aliibuliwa na msanii mkongwe, Seleman Msindi ‘Afande Sele’, mwaka 2003 katika tamasha la kuibua vijana wadogo wenye vipaji lililoandaliwa na kituo cha Redio Ukweli kilichokuwa na makazi yake mkoani Morogoro.

Kipindi hicho akiitwa Dogo Ditto, alishirikishwa kwenye nyimbo zote za albamu ya pili ya Afande Sele iliyokwenda kwa jina la Darubini Kali, ukiwamo wimbo huo wa Darubini Kali

Mwaka 2004, Ditto alimshirikisha Afande Sele katika wimbo wake wa kwanza kurekodi kama msanii anayejitegemea wa Dunia Ina Mambo uliofanikiwa kukamata chati katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Ditto mwaka 2005 alishiriki kuasisi kundi la Watupori akiwa na Afande Sele na Mc Koba baada ya kundi la Ghetto Boys kuvunjika.

Aliachana na Afande Sele na kuungana  na MC Koba wakarekodi albamu yao ya kwanza katika Studio za Bongo Records, ambapo walifanikiwa kutoa wimbo mmoja tu wa Ulibisha Hodi ambao nao ulifanya vyema kabla ya wote kujiunga katika kundi la La Familia lililokuwa likiongozwa na Chid Benz.

Akiwa La Familia, alishirikishwa katika nyimbo kama Ngoma Itambae, Dar es Salaam Stand Up na Muda Umefika na mwaka 2008, Ditto akajiunga na Taasisi ya Kukuza na Kulea Vijana Wenye Vipaji ya Tanzania House Of Talent (THT) ili kujiongezea ujuzi ambapo alifanikiwa kutoa nyimbo kama Wapo, Tushukuru kwa Yote na Niamini.

BINGWA lilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano na Dito kuhusu mafanikio yake pamoja na maisha ya muziki baada ya kutoka THT.

BINGWA: Unatumia mtindo gani wa kutoa nyimbo zako?
Ditto: Ninatoa audio kwanza, naiangalia ikifanya vizuri ndipo natoa na video, natoa ndani ya miezi miwili au mmoja.

BINGWA: Je, unachangia mawazo yoyote katika video zako kabla hazijatoka?

Ditto: Hapana, sijawahi kutoa mawazo yoyote, nikishamaliza kurekodi audio na nikajua imefanya vizuri suala la video namwaachia Director anafanya kila kitu hapa nakuwa sihusiki tena.

BINGWA: Je, ulipotoa wimbo wa Moyo Sukuma Damu ulijua ungekuwa na mapokezi makubwa kiasi kile?
Ditto: Hapana sikujua kabisa, nilijua utakuwa kama nyimbo nyingine lakini nilishangaa kuona mapokezi makubwa kiasi kile, hapo ndipo nilipotambua mashabiki wangu wanataka nini.

BINGWA: Wimbo wa Moyo Sukuma Damu ulijiimbia wewe mwenyewe au?
Ditto: Hapana sijajiimbia mimi, niliimba kutokana na maisha yanavyokwenda kila siku, mambo kama hayo yanatokea kwa marafiki, ndugu zangu. kwahiyo nikaamua kuimba lakini sijajiimbia.

BINGWA: Ni changamoto gani unazokutana nazo katika muziki wako?
Ditto: Zipo nyingi, lakini changamoto kubwa hapa nchini ni mazingira; ukitaka ‘kushuti’ video lazima uombe kibali na ukiomba utapewa zaidi ya miezi miwili, lakini ukienda nje, siku mbili unamaliza kazi zako zote.

BINGWA: Uhusiano wako na THT upoje?
Ditto: Muda wangu mwingi huwa unaishia kule, pale ni sehemu ambayo siwezi kuisahau kwani ndio iliyonifanya nijulikane na nifanye vizuri kwenye maisha pamoja na muziki.

BINGWA: Una mpango wa kufanya kolabo nje?
Ditto: Mpango huo upo, kwanza nimeshafanya na wasanii wawili ila siwezi kuwataja, wimbo umekamilika lakini bado sijautoa, kupitia wimbo wangu wa Moyo Sukuma Damu, wasanii wengi wananitafuta hasa Kenya kwa ajili ya kutoa ‘remix’ ya wimbo huo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*