googleAds

DILUNGA: YANGA MNA BAHATI

NA HUSSEIN OMAR


 

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Hassan Dilunga, amesema Yanga wana bahati kutokana na kukosekana kwake katika mchezo wao wa keshokutwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani alipania mno kuwaonyesha Wanajangwani hao yeye ni nani.

Dilunga, aliyetua Simba msimu huu akitokea Mtibwa Sugar, hatacheza mchezo huo wa keshokutwa utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwa kuwa ni majeruhi.

Akizungumza na BINGWA jana, Dilunga alisema: “Wana (Yanga) bahati sana sichezi Jumapili, nilipanga kufanya kufuru, wangepata tabu sana na wangejuta. Walinitesa sana kipindi ambacho niliichezea timu yao na kuonyesha dharau nyingi kwangu.”

Alisema maumivu ya mfupa wa mguu wa kulia aliyoyapata katika mchezo dhidi ya Prisons ya Mbeya, ndiyo yaliyomfanya kuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili na kuikosa michezo kadhaa ya ligi ambayo timu yake imecheza.

“Haya maumivu niliyapata kwenye mchezo na Prisons ya Mbeya, halafu nikachukulia poa, nikaendelea kucheza, kumbe nilikuwa naharibu zaidi. Ndipo nikaenda hospitali na kupata tiba ya kina zaidi. Mungu akisaidia, baada ya wiki, nitarejea tena uwanjani,” alisisitiza Dilunga.

Dilunga alitua Simba baada ya kuitumikia Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa mafanikio makubwa, ikiwamo kuiwezesha kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania, huku kiungo huyo akiibuka mchezaji bora.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*