Dili zinazosubiriwa kutikisa usajili kiangazi

LONDON, England

HIKI ni kipindi kibaya sana kwa makocha na mabosi wa klabu mbalimbali barani Ulaya, hasa zile zinazohaha kuwazuia mastaa wake wanaotolewa macho na vigogo wengine.


Hata hivyo, hakuna namna ya kutenganisha kipindi hiki na tetesi ambazo kwa upande mwingine zina mvuto mkubwa kwa mashabiki wanaotaka kujua wachezaji wanaowaniwa na timu zao.
Kwa upande mwingine, ni kawaida kwa kila dirisha la usajili kushuhudia dili ambazo hazikutarajiwa kabisa. Je, hizo zinaweza kujitokeza safari hii? Ndiyo.


Alexis Sanchez (Juventus)
Wakali hao wa Serie A wamekuwa wakitajwa kumtaka kwa muda mrefu sasa, lakini safari hii inaweza kuwa tamu kwao kwani naye hana furaha pale Old Trafford.
Kwa mabosi wa Juve, Sanchez anafaa sana kwenda jijini Turin kushirikiana na Cristiano Ronaldo katika eneo la ushambuliaji.


Lakini sasa, ili dili hilo likamilike, lazima Sanchez akubali kupunguziwa mshahara na si huu mnono anaopewa na Mashetani Wekundu.
Ofa ya kurejea Italia inaweza kumvutia nyota huyo kwani huko ndiko alikoanzia ustaa wake akiwa na klabu ya Udinese.


Antoine Griezmann (Man United)
Baada ya kuipotezea ofa ya Barcelona msimu uliopita, inaelezwa kuwa bado Griezmann anajutia uamuzi wake huo na hivi karibuni aliwaambia mabosi wa Atletico Madrid kuwa anaondoka zake.


Kufikia hatua hii, Man United iko mstari wa mbele kuitaka huduma yake, ikielezwa kuwa tayari Barca hawamtolei macho kivile.


Juu ya sababu ya kutaka kuondoka Atletico, ni timu hiyo kung’olewa Ligi ya Mabingwa na ukweli kwamba nyota wenzake, Lucas Hernandez na Diego Godin, watatimka zao.


Neymar (Real Madrid)
Kwa muda sasa, uhamisho wa Neymar kwenda Madrid umekuwa ukizungumziwa, ikikumbukwa kuwa ni tangu nyota huyo alipokuwa Santos.


Lakini, huenda majira ya kiangazi haya yakawa wakati mwafaka kutokana na sababu mbalimbali. Neymar hana furaha pale PSG, ikielezwa kuwa amekuwa akikorofishana na wenzake kikosini.


Baada ya timu hiyo kung’olewa Ligi ya Mabingwa msimu huu, alizidi kuiweka shakani hatima yake klabuni hapo baada ya kuwatolea mbovu makinda, akisema wanajifanya wanajua kila kitu.
Katika hatua nyingine, Madrid wanapaswa kutambua kuwa haitakuwa rahisi kumpata Neymar, watalazimika kuvunja kibubu kweli kweli.


Toni Kroos (PSG)
Si tu Madrid inataka kuongeza sura mpya kikosini, bali pia kuwapiga bei baadhi ya nyota wake ili kusuka kikosi cha kibabe kwa msimu ujao.
Mmoja kati ya mastaa wasio na uhakika wa kuwa Snatiago Bernabeu msimu ujao ni huyo Kroos.


Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail, PSG wameshajisogeza kwake, wakiangalia uwezekano wa kuinasa saini yake kwa euro milioni 68.
PSG wanamwona Mjerumani huyo kuwa ndiye mrithi sahihi wa kiungo wa kimataifa wa Ufaransa, Adrien Rabiot, ambaye kwa muda sasa amekuwa akivumishwa kutaka kusepa jijini Paris.


Paulo Dybala (Liverpool)
Tangu kutua kwa Cristiano Ronaldo, Dybala si sehemu muhimu ya kikosi cha Juventus licha ya jina kubwa alilokuwa nalo Serie A hapo awali.
Inaonekana wazi kuwa Dybala anaweza kulazimisha uhamisho wake kuwa hana uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza cha Juve.


Awali, alikuwa akihusishwa na Real Madrid na Manchester United lakini hivi karibuni ni Liverpool ndiyo yenye nafasi kubwa ya kumsajili nyota huyo mwenye thamani ya euro milioni 100.


Sadio Mane (Real Madrid)
Hii nayo inaweza kutokea. Kabla ya Zinedine Zidane kuondoka, Madrid walimtaka Mane na sasa taarifa hizo zimeibuka upya wiki chache baada ya kocha huyo kurejea.


Mane raia wa Senegal amekuwa tegemeo katika kikosi cha Liverpool, akiiwezesha kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu ikiwa nafasi ya pili, ukiacha kuiepeleka fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.


Huenda Liverpool wakapewa pigo jingine na klabu za La Liga baada ya awali Luis Suarez, Javier Mascherano na Philippe Coutinho kutimkia Barcelona.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*