googleAds

DAREVA WAPEWE SAPOTI KUINUA WAVU NCHINI

NA WINFRIDA MTOI


VYAMA vingi vya michezo ya ndani vimekuwa vikisuasua kufanya mashindano ya michezo yao kutokana na changamoto mbalimbali na kushindwa kukamilisha kalenda zao kwa mwaka.

Mara nyingi vyama hivi vimekuwa vikitoa sababu kubwa kuwa ni kukosa wadhamini wa kusapoti shughuli zao, huku michezo hiyo ikiendelea kudorora.

Michezo mingi ya ndani imekuwa haipigi hatua, kutokana na vyama hasa vya mikoa kuwa nyuma katika kutekeleza majukumu yao, kwa kushindwa kuendesha mashindano kwa wakati unaotakiwa.

Vipo baadhi ya vyama ambavyo vinajitahidi na kuzingatia ratiba za kalenda zao, huku vikijikita zaidi katika kuinua vipaji licha ya kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Kati ya vyama vya michezo vya mikoa ambavyo vimekuwa vikizingatia kalenda yao ya mwaka kwa sasa ni Chama cha Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam (Dareva), ambacho kwa misimu minne mfululizo kimekuwa na ligi ndefu na imara ya mchezo huo.

Dareva walianza ligi ndefu mwaka 2015, wakianza kwa timu chache, lakini kila mwaka zinazidi kuongezeka ambapo msimu huu imeshirikisha timu 16, za wanaume 10 na wanawake sita.

Kitendo hiki kinaonyesha ni jinsi gani wanapiga hatua kwa sababu kuna timu mpya zimeanzishwa za mtaani, tofauti na zile zilizozoeleka zinazomilikiwa na taasisi kama za majeshi.

Kwa hali hiyo, ni wazi wavu kwa Mkoa wa Dar es Salaam, inapiga hatua kwani tofauti na ongezeko la timu, wamekuwa wakipata mialiko ya kwenda kushiriki mashindano katika nchi mbalimbali.

Mfano timu mpya ya Faru ambayo ni mara ya kwanza kushiriki ligi hiyo mwaka huu, imeshaalikwa katika mashindano nchini Rwanda na Kenya, huku baadhi ya wachezaji wakipata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa.

Kwa nilivyofuatilia ligi hiyo kwa kuhudhuria baadhi ya mechi zake, inaonekana wazi ni jinsi gani chama hicho kilivyojipanga kuendeleza mchezo huo kutokana na miongozo waliyojiwekea ya kufuata misingi ya mashindano.

Dareva wameondoa ile hali ya kuendesha ligi ya bora liende, bali wanahakikisha kila timu shiriki inafuata taratibu zote hadi za usajili wa wachezaji na ratiba ya mashindano.

Zipo changamoto zinazojitokeza, lakini wamekuwa wakizitatua kwa haraka bila kuharibu utaratibu wa mashindano au kuleta migogoro kwa klabu husika.

Hata hivyo, bado chama hicho kinahitaji sapoti kutoka kwa wadau wa michezo, ili kufikia malengo ya kukuza mpira wa wavu na kutoa wachezaji wengi  kwa sababu  kwa timu zilizojitokeza inaonyesha wazi vipaji vipo vingi.

Kutokana na mabadiliko uendeshaji michezo kwa sasa, msingi mkubwa wa mashindano yoyote ili yaweze kufanikiwa ni uwepo wa wadhamini, ambao watasaidia upatikanaji wa mahitaji muhimu kwa urahisi.

Licha ya kwamba Dareva wanapiga hatua kwa kujiendesha wenyewe bila uwepo wa mdhamini mkubwa, ni wazi wakipata wadau wakuwasapoti naamini watafika mbali zaidi ya hapo na tutashuhudia mabadiliko makubwa ya mchezo huo.

Kama wameweza kukusanya timu 16 kwa msimu na kuendesha ligi miezi sita, bila ya uwepo wa mdhamini na ushindani umeonekana, je, endapo watapata sapoti ya wadau wengine hali itakuwaje?

Ukiangalia hata viwanja walivyokuwa wakitumia tangu ligi hiyo ianze ambayo inafikia tamati kesho, vilikuwa si vya uhakika na kuwafanya wahame hame kutokana na uwanja wa taifa wa ndani wanaoutegemea kuwa na shughuli nyingi.

Naamini mpira wa wavu ni mchezo ambao unaweza kuitangaza vizuri Tanzania kimataifa kinachotakiwa ni uwekezaji zaidi wa kuibua vipaji na kuwasapoti wale wanaoonyesha nia ya kuuendeleza kama Dareva.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*