Conte amtaja mchawi wake Chelsea

LONDON, England

KOCHA mkuu wa klabu ya Chelsea, Antonio Conte, amefunguka na kusema kwamba kiungo wake, Cesc Fabregas, ndiye anayempa tabu ndani ya kikosi hicho hadi sasa.

Conte hakumpanga Mhispania huyo kwenye kikosi cha kwanza kilichocheza mtanange wa ufunguzi wa Ligi Kuu England, na amekiri kuwa alipata wakati mgumu wa kumpanga kwenye kikosi cha kwanza kilichofungwa mabao 2-1 na Liverpool mapema wikiendi iliyopita.

Kocha huyo alisema kiwango anachokionesha Fabregas kwenye mazoezi ni cha hali ya juu, lakini amekuwa akipata tabu kumpanga na kumpa nafasi kwa kile kinachoonekana kama kukamilika kwa idadi ya viungo wa Chelsea kwenye kikosi cha kwanza.

“Fabregas yupo kwenye mipango yangu na mipango ya Chelsea,” alisema Conte kabla ya kukutana na Liverpool.

“Wote tunatambua kuwa yeye ni mchezaji mzuri, kama akiendelea hivi kwenye mazoezi atanipa wakati mgumu kufanya maamuzi,” aliongeza.

Conte amewapa kipaumbele viungo,  N’Golo Kante na Nemanja Matic, na licha ya kutopewa nafasi kila mara msimu huu, Fabregas amemvutia Conte kwa nidhamu yake akiwa benchi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*