googleAds

Conte aishangaa Inter Milan kuchelewesha dili la Lukaku

MILAN, Italia

INTER Milan wamepata ubaridi, baada ya kuambiwa walipe pauni milioni 75 ili waweze kupata saini ya straika wa Manchester United, Romelu Lukaku.

Suala hilo linaonekana kumchosha kocha wa Inter Milan, Antonio Conte ambaye alimfanya Lukaku chaguo la kwanza kusajiliwa ndani ya kikosi hicho cha mabingwa wa zamani wa Italia.

Hivi sasa straika huyo yupo nchini Singapore na kikosi cha Manchester United ambacho kinajiandaa na msimu mpya baada ya kucheza michezo miwili ya kirafiki nchini Australia dhidi ya Perth Glory na Leeds United.

Lakini inadaiwa kuwa vigogo wa Inter Milan wameshindwa kupeleka ofa nyingine huku wakijiuliza kama kweli Lukaku anaweza kuwa na thamani hiyo ya pauni milioni 75.

Baada ya kumwambia Ole Gunnar Solskjaer kuwa anataka kuondoka, straika huyo wa Ubelgiji amekuwa akiwapasua vichwa mabosi wa Inter Milan ambao wapo tayari kutoa pauni milioni 33 ili kumnasa Rafael Leao anayefukuziwa na Everton.

Hata hivyo, taarifa zinasema kuwa Conte amekuwa mkali kama mbogo, baada ya mabosi wake wapya kushindwa kumsajili Lukaku huku akidai kuwa wanavunja ahadi ya kumpa kila mchezaji anayemtaka.

Conte anataka mastraika wawili ndani ya kikosi chake ambao wanatajwa kuwa Lukaku na Edin Dzeko wa AS Roma huku akimfungulia milango ya kuondoka Mauro Icardi anayetajwa kukujiunga na Juventus.

Kocha huyo raia wa Italia anamtaka Lukaku kama chaguo la kwanza ndani ya Uwanja wa San Siro, maana yake mabosi wa Inter Milan wanatakiwa kufanya kazi zaidi kuishawishi Manchester United imwachie straika huyo.

Mkurugenzi wa Manchester United, Ed Woodward amewaambia Inter Milan watoe pesa bila kujumuisha mchezaji katika dili hilo la Lukaku.

Lukaku mwenye umri wa miaka 26 hajacheza mchezo wowote wa kirafiki ambayo Manchester United wamecheza mpaka sasa ikidaiwa kuwa amepata majeraha ya nyma za paja.

Manchester United atacheza dhidi ya Inter Milan leo katika mchezo wa kirafiki huko nchini Singapore.

Next Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*