Coastal Union yaipeleka Yanga Kamati ya Saa 72


LULU RINGO, DAR ES SALAAM

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Tanzania, Salum Chama, amesema anasubiri ripoti ya kamisaa wa mchezo kati ya Coastal Union na Yanga, mchezo uliochezwa Jumapili, Februari 3 katika Uwanja wa Mkwawani jijini Tanga na kumalizika kwa sare ya 1-1.

Akizungumza na Mtanzania Digital, Chama amesema katika mchezo huo beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, anaweza kufungiwa na Kamati ya Saa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutokana na kumpiga kiwiko Andrew Simchimba wa Coastal Union wakati wa mchezo.

“Tunasubiri ripoti ya kamisaa wa mchezo kujua kama aliona tukio au la, kwa upande wangu niliona kupitia TV (runinga), hivyo kama ataliweka kwenye maelezo lazima litafanyiwa kazi,” amesema Chama.

Mwamuzi aliyechezesha mchezo huo, Nassor Mwinchumu, naye huenda akaingia matatani kwa kushindwa kutafsiri sheria 17 za soka, lakini pia uamuzi wa kamati ya Saa 72 ndiyo yenye mamlaka ya kushughulikia suala hilo.

“Kamati yangu haihitaji kufanya kazi na watu wasio makini, ndio maana mara kwa mara mwamuzi yeyote akibainika kwenda kinyume na kanuni na sheria za soka tunamwadhibu,” aliongeza Chama.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*