COASTAL UNION KUANZA USAJILI U-20

NA OSCAR ASSENGA, TANGA

UONGOZI wa klabu ya Coastal Union, umepanga kuanza na usajili kwa timu ya vijana chini ya miaka ishirini (U-20) wiki ijayo, huku ukiendelea kusaka wachezaji watakaokitumikia kikosi hicho katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Coastal ambayo ilipanda daraja msimu huu kucheza Ligi Kuu baada ya kusota katika michuano ya Ligi Daraja Kwanza (FDL) kwa muda mrefu, inakusudia kuweka mazingira bora ya kuwawezesha kucheza mashindano hayo kwa mafanikio.

Akizungumza na BINGWA jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Steven Mguto, alisema lengo la kuanza na kikosi cha vijana ni kutaka kukiimarisha ili wapate urahisi wa kuchagua wachezaji watakaohitajika kupandishwa kucheza katika timu ya wakubwa.

“Kama unavyojua klabu zinazoshiriki Ligi Kuu zinatakiwa kuwa na timu ya U-20, hivyo kwa sababu hiyo tunakusudia kuanza mchakato huu wiki ijayo na baadaye tutaelekeza nguvu kwenye usajili wa wachezaji watakaocheza timu ya wakubwa,” alisema.

Aidha, Mguto aliongeza kuwa hivi sasa wanasaka wafadhili ambao watawasaidia kwenye harakati za usajili na ushiriki wao katika Ligi Kuu kwa kuwa klabu haina fedha za kuwawezesha kufanya mambo hayo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*