Chonde chonde waamuzi msimu mpya Ligi Kuu unakuja

Na Mwandishi wetu

PANZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara, litafunguliwa rasmi Jumamosi wiki hii, kwa timu tano kuvaana katika viwanja mbalimbali nchini.

Maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu yamekamilika kwa timu nyingi, huku   tayari  mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Azam imechezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 4-2.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hivi karibuni inaonyesha Mbao wataanza kucheza na Alliance kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba, Mwanza, wakati Mbeya City watacheza na Tanzania Prisons, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Namungo watawakaribisha Ndanda kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi na Polisi Tanzania watakuwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi kumenyana na Coastal Union, wakati Biashara United watavaana na Kagera Sugar, Uwanja wa Karume, mjini Musoma.

Tunaamini kuwa timu zote zitaingia uwanjani zikiwa zimefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha zinapata matokeo mazuri na baadaye kuchukua ubingwa wa ligi hiyo.

Tukitarajia burudani zuri kwa mashabiki, BINGWA tunapenda kuona waamuzi wanachezesha Ligi Kuu kwa kuzingatia sheria 17 za soka ili mshindi apatikane kutokana na uwezo wake.

Tumeamua kusema hilo mapema kutokana na malalamiko kutoka kwa mashabiki, makocha, viongozi wa klabu na wadau wengine kuhusu waamuzi kupindisha sheria kwa lengo la kuinufaisha timu moja.

Kwa kuwa waamuzi ndio wanashika mpini ni jukumu lao kuepuka shutuma kwa kuhakikisha wanachezesha kwa haki, bila upendeleo wowote.

Tunasema kuwa, haitakuwa na maana iwapo bingwa wa msimu ujao ambaye ataiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa,  baadaye atapatikana kwa kubebwa na waamuzi na mwisho wa siku tunapata mwakilisha ambaye hana uwezo wa kushiriki michuano hiyo.

BINGWA tunaamini timu ambayo imefanya maandazi mazuri ndiyo ambayo inaweza kupata matokeo bora ingawa katika soka kuna mamba matatu yaani kushinda, sare na kufungwa.

Kwa kuwa mpira unafungwa kutokana na makosa, BINGWA tunasema chonde chonde waamuzi wasisababishe mashabiki kukosa burudani kwa uchezaji ambao hautazingatia sheria za soka.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*