CHIRWA ANATAKA KUREJEA YANGA NJAA IMEISHA?

NA WINFRIDA MTOI

Mshambuliaji  wa zamani wa timu ya Yanga, Obrey Chirwa, juzi aliibuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Wanajangwani hao walipokuwa wanacheza na Alliance FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga juzi iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 yaliyofungwa na Heritier Makambo, Mrisho Ngassa na Ibrahim Ajib.

Chirwa alionekana jukwaani akiwa na viongozi wa klabu ya Yanga ambao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika na Kaimu Katibu Mkuu, Omari Kaya.

Kuonekana kwa Chirwa uwanjani huku kukiwa na tetesi kwamba anafanya mawasiliano na viongozi wa klabu hiyo, inaonyesha wazi huenda anahitaji kurejea katika timu hiyo kutokana na mipango yake kutokwenda vizuri huko alipokuwa.

Baada ya kuachana na Yanga katika kipindi cha usajili wa dirisha kubwa, Chirwa alitimkia nchini Misri ambako alisajiliwa na timu ya Nogotoom, lakini hakuweza kuonyesha makali yake.

Ikumbukwe kuwa licha ya Chirwa kumaliza mkataba na Yanga, kipindi anaondoka bado uongozi wa klabu hiyo ulikuwa unamhitaji ili aendelee kuisaidia timu hiyo katika mechi za kimataifa za Kombe la Shirikisho barani Afrika zilizokuwa zinawakabili.

Baada ya msimu uliopita wa Ligi Kuu kumalizika, klabu ya Yanga ilikuwa katika kipindi kigumu kutokana na wachezaji wengi kumaliza mikataba yao.

Pia hali ya ukata ilisababisha kukosa fedha za kufanya usajili hivyo kulazimika kutumia njia mbadala ya kuwabembeleza nyota wao huku wakiwaomba wadau kuwasaidia.

Katika kipindi hicho baadhi ya wachezaji waliamua kuondoka akiwamo Chirwa aliyekataa kuongeza mkataba kutokana na ukata uliokuwa unaikabili klabu hiyo.

Straika huyo hakutaka kusikia suala la kukosa fedha bali alikuwa akihitaji kupewa chake  pale muda unapofika tofauti na wachezaji wengine waliojitahidi kuwa wavumilivu.

Kabla hajamaliza mkataba wakati Ligi Kuu inaendelea, tulishuhudia Chirwa akigomea  mazoezi na kukataa kucheza baadhi ya mechi na muda mwingine alikuwa akisafiri kwenda nchini kwao Zambia kupumzika.

Kipindi hicho tulishuhudia viongozi wa Yanga wakihaha kumsaka Chirwa hasa wanapokuwa wanakabiliwa na mechi ngumu ili ajumuike na timu lakini wakati mwingine aligoma kabisa.

Lakini pia hata alipokubali kucheza kiwango chake kilionekana kuwa chini tofauti na ilivyozoeleka hali iliyosababisha hata baadhi ya mashabiki kumpigia kelele kwa kudhani anatumika.

Kuna changamoto nyingi ambazo uongozi wa Yanga ulipitia katika kipindi cha mwishoni ambacho straika huyo alikuwa anamalizia mkataba wake hadi klabu hiyo kufikia hatua ya kufikiria kumsajili Adam Salamba.

Wakati huo Salamba alikuwa anaichezea Lipuli FC ya Iringa lakini Yanga walitaka kumsajili ili awasaidie katika michuano ya kimataifa baada ya kuona Chirwa anawasumbua.

Sarakasi za Chirwa na uongozi wa Yanga zilifikia tamati mwishoni mwa Ligi Kuu msimu uliopita na kabla hajaondoka aliomba kulipwa masilahi yake ili akatafute maisha sehemu nyingine na kuamua kutimkia Misri.

Leo hii inaonekana wazi mambo hayajamwendea vizuri mshambuliaji huyo huko alipokwenda kwa sababu hata ukifuatilia rekodi yake tangu alipoondoka hajasikika kama ilivyo kwa wachezaji wengine ambao wametoka timu za Tanzania na kwenda kucheza soka la kulipwa.

Inawezekana hali hiyo imemfanya Chirwa aamue kurejea hapa nchini kwa kuwa ni sehemu pekee iliyofanya jina lake kuwa kubwa kutokana na uwezo wake na kuwa miongoni mwa wachezaji nyota wa kimataifa waliofanya vizuri.

Hakuna tatizo kama Chirwa anataka kurejea Yanga, lakini jambo la msingi la kujiuliza, je, njaa na hali ngumu aliyoikimbia anaamini imekwisha?

Licha ya kwamba inadaiwa nyota huyo anafukuziwa na Azam FC ambao wanataka kumsajili dirisha dogo, lakini pia ukaribu wake na viongozi wa Yanga unaashiria kuna jambo linaendelea.

Lakini pia kama anataka kurejea Yanga anapaswa kutambua kwamba hali ya ukata alioukimbia bado haujaisha bali wachezaji waliopo sasa ni wavumilivu na wanapata matokeo mazuri kutokana na juhudi zao na kujituma.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*