CHILUNDA ATAMBULISHWA RASMI HISPANIA

NA FAUDHIA RAMADHANI             |              


 

ALIYEKUWA mshambuliaji wa Azam FC, Shaaban Idd Chilunda, jana alitambulishwa rasmi katika klabu yake mpya ya Deportivo Tenerife ya nchini Hispania, baada ya kufaulu vipimo vya afya alivyofanya katika Hospitali ya Rambla nchini humo.

Straika huyo alitua nchini Hispania juzi na jana alifanyiwa vipimo ili kukamilisha usajili wake na kujiunga na klabu yake hiyo mpya, inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini humo.

Chilunda, aliyeng’ara na kikosi cha Azam katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita pamoja na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo.

Nyota huyo aliyechipukia katika kikosi cha vijana cha Azam, aliifungia Azam mabao tisa katika Ligi Kuu na kufanikiwa kuibuka mfungaji bora wa michuano ya Kagame, baada ya kutikisa nyavu mara nane.

Akizungumza na BINGWA juzi, Chilunda alisema amefurahi kupata nafasi hiyo ya kucheza soka la kulipwa Ulaya, huku akisisitiza kuwa atapambana kuisaidia Tenerife kupanda daraja.

“Ni furaha kubwa katika maisha, maana nilikuwa na ndoto kwamba siku moja nitakuja kucheza soka la kulipwa Ulaya, sasa nimefanikiwa na ninatumaini vipimo vyangu vya afya vitakwenda vizuri kabla ya kuungana na wenzangu,” alisema Chilunda.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*