CHILUNDA AMFUATA FARID HISPANIA

NA FAUDHIA RAMADHANI

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Shaaban Idd ‘Chilunda’, amepata uhamisho wa kwenda kuichezea timu ya Deportivo Teneriffe inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (Sugunda Division) ya nchini Hispania kwa mkataba wa miaka miwili.

Hatua hiyo inakuja baada ya mazungumzo ya muda mrefu kwa viongozi wa pande zote mbili, kutokana na Azam na Deportivo Teneriffe kuwa na mahusino ya karibu hasa katika uhamisho wa wachezaji.

Chilunda aliliambia BINGWA jana kuwa, tayari amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo mpya ambapo atakaungana na nyota mwenzake, Farid Mussa ambaye pia alitokea Azam.

“Nashukuru kila kitu kimekwendwa sawa chini ya viongozi wangu wa klabu, kilichobaki ni masuala ya vibali tu ikiwamo Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC), kwa kweli nimefurahi sana kwenda kucheza soka nje ya nchi,” alisema Chilunda.

Nyota huyo anaondoka Azam akiwa ni kinara wa mabao msimu uliopita ambapo alifunga mabao tisa pamoja na kutwaa tuzo ya bao bora la msimu.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hans van der Pluijm, ameweka wazi kuwa, chini ya usimamizi wake hakuna mambo ya kubebana ndani ya kikosi hicho mara Ligi Kuu msimu ujao itakapoanza.

Mholanzi huyo alisisitiza kuwa, kila mchezaji atapata nafasi kulingana na uwezo ambao ataoonyesha uwanjani pamoja na nidhamu ya ndani na nje ya uwanja.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Pluijm alisema anachokitaka kwa Azam msimu ujao ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, hivyo kila mchezaji anatakiwa  kuonyesha juhudi ili acheze kikosi cha kwanza.

Alisema pamoja na kupendekeza kusajiliwa kwa wachezaji wenye sifa anazohitaji, haimaanishi kuwa ndio watapewa nafasi kubwa ya kucheza, kwani kama viwango vyao haviridhishi benchi litawahusu.

“Kikubwa ninachoangalia kwa kila mchezaji ni uwezo pamoja na nidhamu, hivyo kama mchezaji hajitumi na hana nidhamu siwezi kumpa nafasi ndani ya kikosi,” alisema Pluijm.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*