googleAds

CHEKIBUDI Mkongwe wa filamu aliyekaa benchi kusubiri soko lisimame YUKO WAPI

NA JEREMIA ERNEST

UIGIZAJI ni sehemu tu ya kipengele katika sanaa ambacho kimeibua mastaa kibao waliojizolea umaarufu kutokana umahiri wao wa kuigiza kulingana na kazi wanazofanya.

Wasanii wengi wenye majina makubwa hapa nchini wameibukia kwenye tasnia hiyo na miongoni mwao ni Mohamed Nurdin ‘Chekibudi’ ambaye pia alikuwa mchezaji wa mpira wa miguu.

Msanii huyu alipata umaarufu zaidi mwaka 1999 wakati akiigiza tamthiliya ya ‘Nani zaidi’ iliyokuwa ikionyeshwa katika kituo cha runinga ya CTN.  

Chekibudi ni miongoni mwa wasanii  waliopata nafasi ya kuonyesha kipaji cha kuigiza akitokea katika mchezo wa mpira wa miguu.

Hata hivyo, umaarufu wake uliongezeka maradufu kutokana na kupenda kuigiza zaidi sehemu za ukorofi na mapenzi.

Chekibudi alizaliwa mwaka 1981 katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam na kusoma elimu ya msingi  Shule ya Ilala Kasulu, baadaye akajiunga na kidato cha kwanza Sekondari ya Markas Islamic iliyopo Chang’ombe, Dar es Salaam.

Lakini hakufanikiwa kumaliza kidato cha nne kwa sababu za kifamilia, hivyo  akaamua kutoroka kwenda nchini Kenya mwaka 1997.

Chekibudi amefunga ndoa na wanawake watatu pia ni baba wa watoto saba.

*Historia katika sanaa

Chekibudi anasema safari yake kwenye sanaa ilianza rasmi mwaka 1999 kipindi anatokea Kenya, ambapo alijiunga na timu ya mpira wa miguu ya Filidaus.

“Tulicheza mechi na kundi la waigizaji nikafanikiwa kufunga bao moja na kuanza kushangilia kwa kumwaga michanga,” anasema.

Baada ya kucheza mchezo mmoja, alifuatwa na Mkurugenzi wa Kundi la Sanaa la Splendid, Kassim Twalib, ambaye alimuomba akaigize nao kuziba pengo la Dk. Cheni aliyekuwa mwigizaji.

Kwa kipindi hicho, Dk. Cheni alikuwa anahama kutoka Kundi la Sanaa la Splendid kuhamia Kaole Sanaa Group kutokana na mwonekano na uchangamfu wake.

Anasema baada ya kukaa Splendid kwa muda mrefu, aliamua kwenda Kundi la Nyota Academia ambako alikutana na waigizaji mahiri kama Jacob Steven ‘JB’, George Tyson (marehemu), Monalisa, Natasha na Single Mtambalike.

Chekibudi anaeleza kuwa kutokana na wasanii hao kuwa na uwezo wa kuigiza, walizidi kumvutia zaidi kuipenda sanaa.

Filamu alizocheza ni Sabrina, Tunu, Riyama, Machozi, Out of Mind, Limbwata, Mimba, Mapito na nyingine nyingi.

*Mafanikio, changamoto

Akizungumzia mafanikio aliyoyapata kupitia sanaa, Chekibudi anasema kitu pekee anachoweza kujivunia kwa sasa ni kujulikana na watu tofauti na pia jina lake limekuwa maarufu.

Anaeleza kuwa sanaa pia ilimwezesha kufungua kampuni yake mwenyewe ya Chekibudi Production.

Akielezea changamoto alizopitia, anasema aliwahi kufanya kwa kujitolea ili tu kipaji chake kionekane.

“Zamani sanaa haikuwa inalipa, nilifanya kazi miaka mitatu kwa kujitolea bila kupata hata nauli ya kwenda eneo la kuigizia,” anasema Chekibudi.

Pia anasema unaweza kutumia gharama kubwa kutengeneza filamu lakini isitoke kwa sababu mbalimbali.

*Kilichompoteza kwenye sanaa      

Kuhusu kupotea kwenye sanaa, Chekibudi anasema aliamua kukaa kimya kwa sababu ya kushuka kwa soko la filamu.

“Soko la filamu limeyumba, hivi sasa si kama ilivyokuwa zamani maana huwezi kufanya kazi isiyokuwa na faida,” anaeleza Chekibudi

Anafafanua kwamba soko la filamu limeyumba kwa sababu ya utandawazi, wasanii hawakujiandaa hivyo unakuta kila kinga’muzi kinaonyesha filamu na tamthiliya mpaka kwenye YouTube.

“Tulizoea kuuza CD lakini hivi sasa mtu akitaka filamu anaangalia kwenye YouTube au king’amuzi kinachoonyesha, hivyo hawezi kufikiria kununua CD,” anasema.

Chekibudi anaongeza kuwa, haonekani kwa upande wa tamthiliya kutokana na wahusika wanaomtaka kufanya naye kazi kushindwa kufikia kiwango anachotaka.

“Nilifuatwa na wahusika wa tamthiliya ya Huba, lakini hatukuweza kukubaliana kutokana na mkataba wao kuwa tofauti na nilichokuwa nakihitaji,” anasema.

*Mipango yake ya sanaa

Mkongwe huyo wa sanaa ya uingizaji, ameieleza safu hii kwamba sasa anaishi Ilala Bungoni Mtaa wa Al-Hamud na familia yake.

Anasema kazi zinazomwingizia kipato kwa sasa ni kusherehesha shughuli mbalimbali (MC), kupika chakula na kufanya video production kwenye sherehe na hafla.

Pia anasema ameandaa filamu tatu za Kisebusebu, Mahari na Ulimi ambazo amezihifadhi akisubiri soko likae sawa ili aziachie.

@@@@@@@@@@@


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*