CHAMA, OKWI WAMPONZA BOSI SIMBA

WINFRIDA MTOI NA DEBORA MBWILO (Tudarco)


MENEJA wa timu ya Simba, Richard Robert, amefungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutojihusisha na soka ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha mwaka mmoja na kulipa faini ya shilingi milioni nne.

Adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya Maadili ya TFF, baada ya meneja huyo kukutwa na makosa mawili, kuihujumu timu ya Taifa, Taifa Stars na kushindwa kutii maagizo ya shirikisho hilo la soka nchini.

Makosa hayo yalitokana na sakata la wachezaji wa Simba kushindwa kujiunga na kambi ya kikosi cha Taifa Stars kwa wakati na kufikia hatua ya nyota wao kuenguliwa kikosini.

Wachezaji hao ni Erasto Nyoni, John Bocco, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Shomari Kapombe na Hassan Dilunga ambao walichelewa kujiunga na kambi ya Stars kujiandaa na mechi ya kufuzu  fainali za Mataifa Afrika (Afcon) dhidi ya Uganda iliyopigwa wikiendi iliyopita jijini Kampala, Uganda.

Baada ya wachezaji hao kuenguliwa kikosini, Robert na Katibu Mkuu wa Simba, Hamis Kisiwa, walipelekwa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo, Hamidu Mbwezeleni, alisema adhabu hiyo imetolewa baada ya pande zote mbili kukutana na kupitia kanuni.

Mbwezeleni alisema kutokana na kitendo cha wachezaji kushindwa kwenda timu ya taifa, kumesababisha mgogoro wa kimasilahi kati ya TFF na Simba.

Alifafanua kuwa adhabu ya kwanza ya kuhujumu timu ya Taifa imetolewa kwa mujibu wa vifungu vya 5(2) na 6(c)&(h) vya kanuni ya maadili ya TFF toleo la 2013, huku ya kutotii agizo la TFF, ikitolewa kwa kifungu cha 41(8), kanuni za Ligi Kuu toleo la 2013.

“Kamati baada ya kupitia maelezo ya Robert, inamtia hatiani kwa kosa la kuihujumu timu ya taifa na kuleta mgongano wa kimasilahi, masilahi ya Simba yanagongana na TFF kwa sababu inakuwaje Simba ina nusu ya wachezaji timu za taifa za nje ya nchi lakini TFF haina barua ya ruhusa.

“Mtu kama Okwi, alikwenda na simu yake na kumuonyesha meneja kuwa anahitajika timu ya taifa na kuruhusiwa, lakini huku Bocco unamkataza, hiyo ni hujuma kwa sababu unamruhusuje Okwi akatumalize halafu kina Bocco umewazuia?

“Hii ni hujuma mbaya, kuna vitu vingi ila tumelichukulia tu kimpira hatuwezi kuweka vyote wazi, hapa tunajaribu kuweka heshima katika klabu zetu, zijue kuwa TFF ndiye kiongozi wa mpira wetu,” alisema Mbwezeleni.

Hata hivyo, alisema Simba bado wanaweza kukata rufaa kuhusu uamuzi uliotolewa dhidi ya kiongozi wao huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*