CANNAVARO WA BONGO ALIYEUTWAA UMENEJA YANGA

NA MWAMVITA MTANDA


*Apania kuimarisha nidhamu kwa wachezaji, kuitumikia timu kwa moyo wao wote

NADIR Haroub ‘Cannavaro’, ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga wenye heshima ya kipekee kutokana na jinsi alivyoitumikia timu hiyo kwa nguvu, uwezo na moyo wake wote.

Tangu ametua Yanga mwaka 2006, Cannavaro hajawahi kuihama timu hiyo hata pale ilipokuwa katika wakati mgumu tofauti na ilivyokuwa kwa nyota wengine wa klabu hiyo kama Edibily Lunyamila, marehemu Said Mwamba ‘Kizota’, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ na wengineo wa aina yake.

Ukiachana na uchezaji wake wa jihadi kuipigania timu katika michuano mbalimbali, Cannavaro akiwa kama nahodha wa timu, alikuwa ni zaidi ya kiongozi ndani ya kikosi cha Wanajangwani hao.

Ni kutokana na hilo, ilitokea wakati fulani hata aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, alikuwa tayari kuzungumza na Cannavaro juu ya mambo yanayoihusu timu huku akiwakacha baadhi ya viongozi.

Mathalani, mara baada ya kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti, viongozi wa Yanga walikuwa wakihaha kumsihi bosi wao huyo kujiuzulu, lakini kuna wakati hakutaka kuwapa muda wa kuzungumza nao.

Lakini kila Cannavaro alipoomba kukutana naye, Manji hakuwa na kipingamiza na kuzungumza na nahodha huyo.

Ikumbukwe kuwa Cannavaro ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga walioitumikia timu hiyo na hata Taifa Stars kwa muda mrefu zaidi, huku makocha wote waliowahi kuifundisha timu hiyo wakionekana kumkubali.

Hatimaye, baada ya kuitumikia Yanga kwa muda mrefu, umri umeanza kumtupa mkono Cannavaro na inaonekana wazi akili yake inataka kucheza mpira lakini mwili ukikataa.

Uongozi wa Yanga umeliona hilo na kuamua kumpa cheo cha Meneja wa timu yao kuchukua nafasi ya Hafidh Saleh.

Hivyo, msimu ujao Cannavaro hatakuwa katika orodha ya wachezaji waliosajiliwa Yanga, zaidi ya kutambulika kama meneja.

BINGWA limezungumza na Cannavaro kuelezea jinsi alivyojiandaa kuitendea haki nafasi yake hiyo mpya na Mzanzibari huyo kuzungumza mengi, ikiwamo matarajio yake ndani ya Wanajangwani hao.

“Ninayo matarajio makubwa sana katika klabu yangu, lakini kikubwa kutekeleza yale ambayo natakiwa kuyafanya kwa nafasi niliyopewa, hii ni nafasi muhimu kwangu na sikuwahi kutarajia kama nitaipata, pia natoa shukrani zangu kwa kamati iliyokaa na kunifikiria kuwa nitaweza,” anasema Cannavaro.

Cannavaro anasema kikosi cha Yanga kikiwa chini ya uongozi wake, kitakuwa na tofauti kubwa, ukizingatia tayari alishadumu katika timu hiyo kwa miaka mingi, hivyo anafahamu mbinu zitakazoweza kuiwezesha timu kuwa katika sehemu nzuri.

Aidha, anasema katika klabu hakukosekani changamoto, lakini kama alifanikiwa kukabiliana nazo akiwa mchezaji, hatashindwa kuzitatua akiwa kama kiongozi.

Beki huyo aliyewahi kuvaana na washambuliaji waliowahi kutamba duniani kama Samuel Eto’o, Didier Drogba na wengineo, akiwa na kikosi cha Taifa Stars, anasema ataitumia fursa hiyo mpya aliyopewa kuhakikisha wachezaji wao wanakuwa wavumilivu  ili kufanikisha malengo ya timu yao.

Hata hivyo, Cannavaro anakiri kuwa na kibarua kizito kuhakikisha anaweka mambo sawa ndani ya kikosi hicho, hasa kwa kipindi hiki kinachoonekana kuwa kigumu mno kwao kiuchumi.

“Kwa upande wangu, nitaitumia nafasi hii kuhakikisha ninaweka sawa mambo yaliyokuwa yanaleta shida msimu uliopita, nina imani endapo kama viongozi tutakuwa kitu kimoja, mambo yote yatakuwa sawa,” anasema Cannavaro.

Anasisitiza: “Matumaini yangu ni kwamba viongozi wenyewe ndio wanaweza kufanya timu iwe na masimamo au kuyumba kwa sababu kila jambo lipo mikononi kwao, nitaweza pia kuitumia nafasi hii hata kukaa na viongozi wenzangu kujadiliana tutakavyoijenga timu yetu.”

Cannavaro amewataka wachezaji wa timu hiyo kufahamu kuwa hakuna jambo rahisi, hivyo wanatakiwa kuwa wavumilivu ili kutimiza malengo yao.

Anasema iwapo asingekuwa mvumilivu, leo hii asingepata nafasi hiyo ya umeneja wa timu.

“Napenda pia kuchukua nafasi hii kuwashauri wachezaji, hasa hawa vijana ambao bado hawana miaka mingi katika soka, wajaribu kuwa wavumilivu, mwisho wa siku watayaona matunda yake, si mchezaji akiona timu imeyumba kidogo, anataka kukuhama, matatizo yapo kila sehemu,” anasema Cannavaro.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*