CANNAVARO ASAHAU CHEO CHAKE

MENEJA mpya wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amejikuta akisahau cheo chake hicho na ‘kukirejesha’ kwa Hafidh Saleh.

Saleh amekuwa akishikilia cheo hicho kwa muda mrefu mno tangu wakati Cannavaro alipokuwa akiitumikia Yanga kama mchezaji na nahodha.

Jana baada ya mazoezi yaliyofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia mjini hapa, Cannavaro alijikuta akimwita Saleh meneja, cheo ambacho ni chake.

Kitendo hicho kiliwafanya baadhi ya mashabiki na viongozi wa Yanga kuangua kicheko wakiamini Cannavaro bado hajazoea cheo chake hicho kipya.

Hivi karibuni, uongozi wa Yanga ulimpa Cannavaro cheo hicho baada ya nyota huyo kustaafu soka, huku Saleh akipewa nafasi ya Mratibu wa Timu.

Cannavaro alichelewa kuungana na timu mjini hapa kutokana na kuuguliwa na mama yake akiwa ametua juzi usiku.

Kikosi cha Yanga kimejichimbia mjini hapa katika Hoteli ya Kings Way, Msamvu kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini pia mechi zao mbili zilizobaki za Kombe la Shirikisho Afrika.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*