googleAds

Caf yasogeza mbele mechi ya Simba, JKT Tanzania

WINFRIDA MTOI

Mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na JKT Tanzania, iliyokuwa imepangwa kuchezwa Agosti 23, imesogezwa mbele hadi Agosti 29, mwaka huu, kutokana na mwingiliano ya michuano ya Kimataifa.

Kwa mujibu wa ratiba ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Simba watakuwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, kucheza na UD Songo ya Msumbuji katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na BINGWA juzi, Kocha wa timu ya JKT Tanzania, Abdallah Mohammed ‘Bares’, alisema wamepata barua kuwa mechi yao na Simba itachezwa Agosti 29, hivyo hakuna kitakachoharibika.

Bares alisema kutokana na mabadiliko ya ratiba hiyo wataendelea kutumia muda uliopo kufanya maandalizi wakiwa kambini Zanzibar, ikiwamo kucheza mechi nyingi za kirafiki.

“Sisi mechi ya ligi tunaanza tarehe 29 badala ya 23, kwa sababu Simba wana mchezo wa Ligi ya Mabingwa, tutapata muda mwingi wa kujiandaa,” alisema Bares.

Kocha huyo, alisema tayari wamecheza mechi moja na Zimamoto na kufungwa mabao 2-0 na kesho watacheza na Mafunzo.

“Kwa sasa program niliyokuwa nayo ni kuangalia zaidi eneo la ulinzi likae sawa, umeona mechi ya kwanza tumefungwa, ina maana kuna tatizo, nikikaa vizuri nitaangalia eneo lingine,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*