googleAds

BODI YA LIGI YATANGAZA VITA KWA WAAMUZINA WINFRIDA MTOI

BODI ya Ligi Tanzania Bara (TPLB), imeweka wazi kuwa inaendelea kuwafungia waamuzi wanaofanya makosa ya kushindwa kutafsiri sheria 17 za mchezo wa soka hadi watakapokaa sawa.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Boniface Wambura, wakati akitoa taarifa za Kamati ya Uendeshaji na usimamizi wa Ligi, baada ya kupitia matukio ya mechi zote za raundi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Baada ya wiki iliyopita Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Salum Chama, kutoa taarifa ya kufungiwa na kuonywa kwa baadhi ya waamuzi walionekana kushindwa kumudu michezo yao na kufuata sheria 17 za soka, jana Wambura alitoa uamuzi waliochukua.

Akizungumza na waandishi wa habari, Wambura alisema kufungiwa kwa waamuzi kutaendelea kila bada ya mechi kwa wale ambao watashindwa kumudu michezo wanayopewa kuchezesha.

Alisema msimu huu wana waamuzi wengi na wanataka kila anayepewa mechi, afuate sheria 17 za soka.

“Tumeanza mapema kuwafungia waamuzi ili itakapofika katikati ya ligi wawe wamenyooka na makosa mbalimbali kupungua, hatutakuwa na pengo hata tukiwafungia kwa sababu wameandaliwa wengi,” alisema Wambura.

Wakati huo huo, klabu ya Mbao FC imepigwa faini ya sh.500,000, kutokana na mashabiki wao kuingia katika uwanja baada ya mechi kumalizika, huku wakiwa mabango ambayo hayakuwa na ujumbe mzuri.

Nayo Costal Union faini ya 500,000 kwa mashabiki wao kuingia uwanjani baada ya mechi yao na Lipuli FC, pia walimwandikia barua ofisa usalama wa klabu hiyo, kumueleza  kuwa mashabiki hawaruhisiwi kuingia uwanjani wakati mchezo ulimalizika.

Alisema wamechukua hatua ya kumuandikia barua ofisa huyo kwa sababu vitendo vya mashabiki wa Coastal Union, kuingia uwanjani vimekuwa vikijitokeza mara nyingi.

Klabu nyingine iliyopigwa faini ya sh. 500,000  ni Tanzania Prisons, kutokana na mashabiki wake  kuvamia getini na kutaka kuingia uwanjani bure katika mechi yao dhidi ya Mtibwa Sugar huko Manungu, Morogoro.

Aidha klabu za Yanga, Mtibwa Sugar, Singida United, zilipewa onyo kali kwa kushindwa kuwasilisha orodha ya majina ya wachezaji katika kikao cha asubuhi cha maandalizi ya mechi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*