BOCCO AMCHONGEA OKWI KWA MMACHINGA

NA SAADA SALIM    |  

KITENDO cha mshambuliaji wa Simba, John Bocco, kukubali kumwachia Emmanuel Okwi kupiga mipira yote ya adhabu ikiwamo na penalti, kimeonekana kumchonganisha Mganda huyo na nyota wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’.

Mmachinga ndiye anayeshikilia rekodi ya kupachika mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufunga mabao 26 miaka 19 iliyopita, rekodi ambayo mpaka sasa haijavunjwa na mchezaji yeyote hapa nchini.

Na sasa wawili hao wamekubaliana na kuja na kampeni hiyo ya kutaka kuivunja rekodi ya Mmachinga kwa Bocco kumwachia Okwi apige penalti zote na mipira ya adhabu kwa ajili ya kujiongezea idadi ya mabao ya kufunga.

Okwi mwenye mabao 19, ameizidi rekodi ya Boniface Ambani wa Yanga aliyefunga mabao 18 msimu wa 2008/2009, Musa Hassan Mgosi, (2009/10) na Mrisho Ngassa (2010/11).

Mshambuliaji huyo wa Simba ana idadi sawa na washambuliaji watatu waliofunga mabao 19 katika misimu tofauti, ambao ni Msomalia Isse Abushir msimu wa 2004/05, John Bocco (Azam) 2011/12 na Amis Tambwe (Simba) msimu wa 2013/14.

Pia, Mganda huyo anahitaji bao moja kuivunja rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma, aliyefunga mabao 20 msimu wa 2005/06, endapo atafunga mabao mawili Okwi ataivunja rekodi wa msimu wa 2015/16 ya mabao 21 iliyowekwa na Tambwe wa Yanga.

Nyota huyo kipenzi cha mashabiki wa Simba, tayari amevunja rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga Saimon Msuva, ambaye kwa sasa anakipiga Difaa El Jadid pamoja na Abdulrahman Mussa (Ruvu Shooting) waliofunga mabao 14 kila mmoja msimu uliopita.

Akizungumza na BINGWA jijini, Okwi alisema hana presha na wapinzani wake wanaomkimbiza katika mbio za ufungaji bora kulingana na anayemfuata Bocco mwenye mabao 14 wanacheza pamoja, kwamba atamwachia endapo watapata penalti katika michezo yao iliyobakia.

Alisema licha ya msimu huu timu yao inatwaa ubingwa wa ligi hiyo, lakini pia Bocco anahitaji Mganda huyo kuhakikisha anafanikiwa kufunga idadi kubwa ya mabao na ikiwezekana kumpita mshambuliaji wa Yanga, Mmachinga.

“Ni kweli ligi ni ngumu, lakini kwa upande wetu na Bocco tayari tumeshaweka mikakati yetu kwamba kama tukifanikiwa kupata penalti, basi nitaipiga ili kufikia kile kinachotarajiwa na Wanachama wa Simba,” alisema.

Okwi alisema bado kutofikiria kuchukua kiatu cha ufungaji bora na kulenga ubingwa, lakini tayari Bocco amembashiria na kumhitaji kutwaa tuzo hiyo kwa kufunga idadi kubwa ya mabao ikiwezekana atikise wavu mara 26 kufikia idadi ya Mmachinga aliyefunga miaka 19 iliyopita ambayo hadi sasa haijafikiwa na yeyote.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*