Boban atuma ujumbe mzito Yanga

NA HUSSEIN OMAR

KIUNGO mpya wa Yanga, Haruna Moshi ‘Boban’, amewaambia mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na shaka naye badala yake, wamwombee ili aweze kuwapa kile wanachokitarajia kutoka kwake.

Boban ametua Yanga katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo akitokea African Lyon ambapo usajili wake umewagawa mashabiki wa soka nchini wakidai kuwa kiungo huyo hana jipya kwa madai ni mkongwe.

Akizungumza na BINGWA jana, Boban aliyewahi kutamba akiwa klabu za Simba na Coastal Union, alisema: “Tuombe uzima, hakuna kingine, najua wapi nilikosea… nasisitiza tena, waniombee uzima, sina mengi ya kusema, tukutane uwanjani.”

Boban ambaye si mzungumzaji hasa kwa vyombo vya habari, amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miezi sita, ikiwa ni mapendekezo ya Kocha Mkuu wa Wanajangwani hao, Mwinyi Zahera.

Zahera alivutiwa na Boban baada ya kumshuhudia akifanya vitu vyake wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu yake ya African Lyon na JKT Tanzania.

Akimzungumzia mchezaji huyo aliyewahi pia kutamba akiwa na timu ya Taifa, Taifa Stars, Zahera alisema kuwa anaamini Boban ataongeza kitu katika kikosi chake kilichopo kileleni mwa Ligi Kuu Bara kwa sasa kutokana na kipaji chake, hasa katika suala zima la kumiliki mpira.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*