BFT KUHAMASISHA NDONDI KWA WANAWAKE

NA MWAMVITA MTANDA

UONGOZI wa timu ya Taifa ya wanawake ya ngumi za ridhaa, umesema kwamba, sasa upo katika mkakati mzito wa kuhakikisha kuwa wanapata idadi kubwa ya wanawake wanaoshiriki mchezo huo.

Timu hiyo kwa sasa ina zaidi ya wanawake 30 wenye uwezo wa kukabiliana na mchezo huo na tayari wamefanikiwa kushiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na BINGWA jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Makore Mashaga, alisema kutokana na mwamko uliopo sasa kwa wanawake kupenda michezo, wanachukua fursa hiyo kuhamasisha zaidi ili kupata idadi kubwa.

“Tumeona kwa sasa wanawake wana mwamko wa michezo, hiyo kwetu ni fursa na tutaitumia kuhakikisha kuwa tunaibua vipaji vingi vya mabondia wa wengi wa kike hapa nchini,” alisema Mashaga.

Aidha, Mashaga alisema mbinu watakazotumia kuhamasisha mchezo huo kwa wanawake ni kuandaa matamasha sehemu mbalimbali ili kila mmoja apate fursa ya kushuhudia bila gharama yoyote.

Aliongeza kuwa zoezi hilo litaanza mapema Juni mwaka huu ambapo kwa sasa wapo katika mchakato wa kupanga bajeti ambayo itawasaidia kwenye zoezi hilo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*