BERNARD ARTHUR… KIFAA KIPYA AZAM KILICHOPANIA KUZIMA REKODI ZA KIPRE TCHETCHE

NA MAREGES NYAMAKA

TANGU aondoke mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Tchetche, kwenye timu ya Azam FC, hajatokea mpachika mabao mwingine wa kigeni mahiri kama yeye.

Baadhi ya washambuliaji wa kigeni ambao wamepita Azam na kushindwa kufuata nyayo za Tchetche ni Alan Wanga (Kenya), Francisco Zekumbawira (Zimbabwe), Mohamed Yahaya na Samuel Afful (Ghana).

Lakini sasa wamemnasa mshambuliaji mwingine wa Ghana, Bernard Arthur, ambaye baada ya kusikia rekodi za Tchetche amepania kufuata nyayo zake.

Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdul Mohamed, ndio alikwea pipa hadi Ghana kisha kumalizana na mshambuliaji huyo, Arthur, akimsainisha mkataba wa miaka miwili ingawa dau lake halikuwekwa wazi.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 20, aliyekuwa akiitumikia timu ya Ligi Kuu Ghana, Liberty, ameifungia mabao 11 katika mechi 19 aliyocheza.

Arthur ambaye ni mchezaji pekee aliyesajiliwa Azam katika usajili wa dirisha dogo, alitua Azam kuziba nafasi ya nyota mwenzake wa Ghana, Mohamed Yahaya, aliyetupiwa virago baada ya kushindwa kung’ara.

Tayari nyota ameanza vizuri kwenye timu yake hiyo mpya, baada ya kufanikiwa kufunga bao mchezo wake wa kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Stand United, ambao waliibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Akizungumza na BINGWA, Athur aliyekabidhiwa jezi namba tisa iliyokuwa ikitumiwa na nyota mwingine wa Ghana, Samuel Afful, ambaye naye alichemka, alifunguka mambo mengi ikiwamo malengo yake na namna ya kukabiliana na changamoto za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Apagawa na miundombinu

Moja ya kitu ambacho kimeonekana kumvutia mchezaji huyo na kumpa hamasa ya kufanya kazi ni uwekezaji uliofanywa na klabu ya Azam yenye mwonekano wa kisasa kila idara.

“Nimefurahi sana kuwapo hapa (Azam), kiasi kikubwa nimevutiwa na miundombinu ya klabu hii kwani ni klabu chache sana za Afrika hasa upande wa Afrika Mashariki na Kati kufanya kama hivi, hili linanifanya nihamasike kutimiza majukumu yangu,” anasema Arthur.

“Kuna bwawa la kuogelea, viwanja viwili vya mazoezi, vyote vikiwa na ubora wa juu, ‘gym’, makazi ya wachezaji lakini pia mandhari yenyewe ni rafiki kwa mchezaji yeyote kuwepo hapa.”

Atekwa na sera ya vijana

Sera ya Azam ya kikosi chao kuwa na idadi kubwa ya wachezaji vijana wakiwamo kutoka timu zao za vijana nacho ni kivutio kingine kwa Bernard.

“Nilipofika nikaona wachezaji wengi hapa vijana ambao wanapenda kujifunza na kupambana kuweza kupata mafanikio.”

Aahidi kusaka  rekodi za Tchetche

Baada ya kufahamishwa historia ya mchezaji wa zamani wa Azam, Tchetche, ambaye ni mshambuliaji aliyeifungia Azam mabao mengi kwa upande wa wageni, Bernard alivutiwa na kutaka kuzifunika rekodi hizo.

Tchetche alikuwa mfungaji bora msimu wa 2012/13 kwa kupachika mabao 17 na msimu uliofuata akanyakua tuzo ya mchezaji bora wa kigeni na kuiwezesha Azam kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza na ya pekee msimu wa 2013/14.

“Ni kitu kizuri alichokifanya kama mchezaji wa kigeni, binafsi kwa jitihada zangu na kufuata misingi ya soka nitajitahidi hadi nikiondoka niwe nimeacha rekodi zangu nzuri au zaidi ya zile za Tchetche.”

Lugha kikwazo

Arthur anasema changamoto kubwa anayokumbana nayo ni lugha ya Kiswahili ambayo wachezaji wengi ni wazawa na ndiyo lugha wanayotumia sana.

“Natamani kujichanganya kwa kila mchezaji kushauriana mambo mbalimbali hasa yahusuyo soka, lakini changamoto kubwa ni lugha, lakini wapo Waghana wenzangu ambao tunaongea lugha ya nyumbani,” anasema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*