googleAds

Berahino afurahia umoja kikosi cha Burundi

DOHA, Qatar

NYOTA wa timu ya taifa ya Burundi, Saido Berahino, amesema umoja katika kikosi chao ni chachu ya kufanya vizuri katika Kombe la Afrika nchini Misri. 

Akitumia ukurasa wake wa Instagram, Berahino aliyezaliwa Agosti 4 mwaka 1993 aliandika, “Umoja umekuwa chachu ya mafanikio yetu.” 

Sare ya bao 1-1 dhidi ya Gabon katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Prince Louis Rwagasore jijini Bujumbura ilitosha kuwafanya Burundi kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Mali na kufuzu kwa mara ya kwanza michuano ya AFCON.

Intamba Mu Rugamba kama wanavyofahamika wameweka kambi jijini Doha, Qatar tangu Juni 3 mwaka huu na wapo Kundi B pamoja na mabingwa mara tatu wa AFCON Nigeria, Guinea na Madagascar.

Berahino ni miongoni mwa wachezaji 28 waliyoitwa kikosini na kocha Olivier Niyungeko aliyemiminia sifa straika huyo anayekipiga England akiamini atatengeneza muunganiko mzuri na straika mwingine wa kikosi hicho, Gael Bigirimana, anayecheza soka la kulipwa nchini Scotland.

Burundi watacheza mechi ya kwanza ya kujipima nguvu dhidi ya Algeria kesho nchini Qatar kabla ya kusafiri kwenda Tunis kuwakabili wenyeji Tunisia katika mchezo mwingine wa kirafiki Juni 17.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*