googleAds

Ben Pol: TID ni mtu ‘special’ sana kwangu

Mwandiahi Wetu

KARIBU msomaji wa Jiachie na Staa Wako, safu inayokupa nafasi ya kusoma majibu ya watu maarufu ambao wameulizwa maswali mbalimbali. Leo tupo na Bernard Paul ‘Ben Pol’ anayetamba na wimbo wake mpya, Ebenezer.

SWALI: Isaya Mbago kutoka Mikongwi, anauliza: “Umesafiri sana nchi za watu ni jambo gani limewahi kukutoa ushamba?”

Ben Pol: Nikiwa Marekani niliingia kwenye saluni ya kike bila kujua na nilishafanya ‘booking’ ikabidi ninyoe upara sababu hata lugha walikuwa hawajui Kingereza pia kuna tukio lingine lilitokea Ujerumani.

Nilikuwa kwenye matembezi na rafiki yangu Emmanuel akiwa na mke wake. Kuna Mjerumani mmoja alipita na gari akaongea Kijerumani na wakanipa tafsiri kuwa ni neno la kibaguzi.

SWALI: Constatino John kutoka Vingunguti, anauliza: “Kitu gani kinakuudhi mtandaoni, hasa Instagram?”

Ben Pol: Kama Instagram isingekuwa chombo cha biashara na kujitangaza, nisingekuwepo kabisa mtandaoni, kwa sababu watu wanaandika mambo mabaya, dua mbaya… mtu anatumia nafasi hiyo kukufanya usijione kitu, nipo mtandaoni sababu tu ya kujitangaza, kuna uhuru ambao unaleta hali mbaya.

SWALI: Dwese Yange wa Simiyu, anauliza: “Ulivyokuwa Marekani ulikuwa unakutana na mastaa wakubwa kama kina T.I, Gucci Mane na wengineo, je kuna kazi yoyote itakuja na hao mastaa wa mbele?”

Ben Pol: Nimeongea na T.I, alikuwa anataka hata aone Instagram yangu, Gucci Mane hatukuongea sana kwa sababu katika ile shughuli tuliyokuwepo, wote tulikuwa V.I.P ila kilichotokea ni kwamba Gucci alikuwa kama mgeni wa heshima, niliongea naye kidogo sana muda mwingi niliongea na meneja wake ambaye aliniambia siyo siku nzuri ya kuongea kuhusu muziki sababu alikuwa bize sana.

SWALI: Rajab Abubakari wa Dar es Salaam, ila kwasasa yupo Dodoma, anauliza: “Ulichukuliaje TID kusema wewe ni msanii ambaye hakuelewi baada ya kutoa orodha ya wasanii wako unaowakubali?”

Ben Pol: TID hakuwepo kwenye orodha yangu ya wasanii ninaowakubali kwa sababu yeye ni mtu spesho sana, ana nafasi yake spesho kwa sababu yeye ndiye alinipa jina la Ben Pizzey, yeye ndiye alipandikiza ile RnB ndani yangu, mimi nilikuwa naimba nyimbo zake za albamu yake ya Sauti ya Dhahabu kabla sijatoka kisanaa.

SWALI: Abirah Topwison wa Bagamoyo, anauuliza: “Vitu gani huwa unaviona kwenye tasnia za muziki kwenye nchi za wenzetu na Tanzania havipo?”

Ben Pol: Nilipokuwa Marekani wale madereva wa uber nilikuwa nawauliza sana maswali nikaja kugundua kwamba wenzetu kwenye upande wa kununua muziki ‘digital’, wana heshima sana, unakuta mwananchi wa kawaida kabisa yupo mtandaoni, analipa kila mwezi dola kadhaa kununua muziki ‘online’, hiyo inafanya wanamuziki wa kule wanapata kipato kikubwa, angalau Kenya wanajitahidi.

SWALI: Stumai Daniel wa Mbalizi Mbeya, anauliza: “Kwanini sasa hivi umetoa wimbo wa Injili (Gospel)?”

Ben Pol: Mimi mwenyewe nina stori nyingi sana na Mungu kwa sababu amenipitisha kwenye matukio mengi ambayo bila yeye huenda kikawaida nisingepita. Tangu nimezaliwa mama yangu ananisimulia mambo mbalimbali, mwenyewe nikikumbuka shule kuna matukio ambayo nikikuelezea utashangaa, huko kote kuna Mungu ndiyo maana nikatoa wimbo huo wa kumshukuru.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*