BEKI INTER AMPONDA RONALDO, AMPA TANO MBAPPE

ROMA, Italia


 

BEKI wa Inter Milan,  Stefan de Vrij, ni kama amemchokoza straika mpya wa  Juventus, Cristiano Ronaldo, akisema kwamba licha ya kuwa ujio wake utaongeza msisimko katika michuano ya Ligi Kuu ya Italia, Serie A, lakini hana makali kama ya straika wa Paris Saint Germain, Kylian Mbappe.

Ronaldo alijiunga na Juve akiwa tayari ameshapata mafanikio na Real Madrid katika kipindi cha miaka tisa aliyoitumikia yakiwamo ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne.

Kutokana na ujio huo, wengi wamekuwa wakiamini kuwa Ronaldo anaweza kumaliza ukame wa mataji makubwa Ulaya ambao umeikumba kwa muda wa miaka 22.

Hata hivyo, staa huyo mwenye umri wa miaka 33, ameianza michuano ya Serie A kwa kusuasua na mpaka sasa hajaweza kufunga bao katika michezo mitatu jambo ambalo linamfanya De Vrij  kutokuwa na hofu naye.

“Kusema ukweli mwanzo sikuamini kama anakuja Italia,” Mholanzi huyo aliuambia mtandao wa Corriere dello Sport.

“Lakini baada ya vyombo vya habari kuanza kulizungumzia hilo ndipo nikaanza kufuatilia. Kwa kutua katika soka la Italia kutasaidia kuleta msisimko katika michuano ya Serie A. Nimewahi kucheza naye akiwa na timu ya taifa katika mechi ya kirafiki dhidi ya Ureno kabla ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 na tukatoka sare ya 1-1 na yeye akafunga kwa kona,” alisema beki huyo.

“Sioni kama Ronaldo anaweza kunisumbua sana kama Mbappe licha ya kuwa bado ana miaka 19,” aliongeza  staa huyo.

Akijibu swali kuhusu ni straika yupi ambaye anamhofia, beki huyo mkongwe alizidi kusisitiza zaidi kuwa ni Mbappe.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*