Beki hatari afunguka kutua Jangwani

NA WINFRIDA MTOI

BEKI wa Polisi Tanzania, Yassin Mustafa, ameweka bayana kuwa muda wowote Yanga wakikamilisha yale anayoyataka, anatua Jangwani.

Yanga ilitaka kumsajili beki huyo ili kuziba pengo la Gadiel Michael kipindi cha dirisha dogo baada ya Muharami Issa ‘Marcelo’ kushindwa kuonyesha makali, lakini mkataba ulimbana.

Baada ya Wanajangwani hao kumkosa nyota huyo ambaye alikuwa chaguo la kwanza, walimsajili Adeyum Saleh ambaye naye bado hajaweza kuonesha kiwango kinachoridhisha, huku akisumbuliwa na majeraha.

Kutokana na ripoti ya Kocha Mkuu Luc Eymael, kuhitaji beki wa kushoto, Yanga imeanza tena harakati za kunasa saini ya Mustafa.

BINGWA lilimtafuta beki huyo na kukiri kuwa aliwahi kuzungumza na viongozi wa Yanga, lakini hawakufikia makubaliano, hivyo kama watakamilisha kile anachohitaji yupo tayari.

Mustafa alisema kuwa yeye ni mchezaji na alishazungumza na Yanga tangu dirisha dogo, hawezi kukataa kuchezea timu kama hiyo, anachotaka ni kutimiziwa maslahi yake.

“Ni kweli Yanga niliwahi kuongea nao kuhusu usajili, walikuwa wananitaka kipindi cha dirisha dogo, lakini kuna mambo tulishindwana, kama wapo tayari tena mimi sina tatizo.

Unajua mimi ni mchezaji kazi yangu soka,  nipo tayari kucheza timu yoyote endapo tutafikia makubaliano ya kimaslahi na ninajiami naweza kucheza popote,” alisema Mustafa.

Alisema hakuna hana kizuizi chochote kwa sababu mkataba wake na Polisi unafikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*