BECKHAM NA WANASOKA WENGINE WANAOMILIKI TIMU ZAO

LONDON, England

LICHA ya kustaafu tangu mwaka 2013, jina la David Beckham, limeendelea kuchukua nafasi katika ulimwengu wa soka.

Mbali ya maisha yake ya ‘kula bata’, ni kutokana na kitendo chake cha kumiliki klabu ya soka ya Inter Miami CF ambayo bado haijaanza rasmi, lakini imeshajizolea umaarufu mkubwa.

Tayari imeelezwa kuwa Beckham anataka kuutikisa ulimwengu wa kandanda kwa kuwasajili mastaa, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Hata hivyo, Beckahm si mwanasoka pekee anayemiliki klabu ya kandanda. Makala haya yanakuibulia wengine ambao huenda hukuwafahamu.

Didier Drogba (Phoenix Rising)

Phoenix Rising ni klabu ya Ligi Daraja la Pili nchini Marekani na ilimsajili Drogba mwaka jana. Baadaye, Drogba alinunua sehemu ya hisa klabuni hapo. Mbali ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Chelsea, wamiliki wengine wa Phoenix Rising ni Brandon McCarthy, DJ Diplo, na Pete Wentz.

Giggs, Scholes (Salford City)

Si hao tu, Salford City inamilikiwa pia na Gary Neville, Phil Neville na Nicky Butt, waliowahi kucheza na Ryan Giggs na Paul Scholes, pale Manchester United.

Salford City inashiriki Ligi Daraja la Tano England na nyota hao waliinunua mwaka 2014 ikiwa Ligi Daraja la Saba.

Nyota hao wanne wanamiliki asilimia 50 na sehemu ya hisa iliyobaki wamemuuzia bilionea wa Singapore, Peter Lim, ambaye pia ndiye anayeimiliki Valencia ya La Liga.

Paolo Maldini (Miami FC)

Licha ya kuwa ndiye mkurugenzi wa mikakati na maendeleo ya soka katika klabu ya AC Milan, Maldini anamiliki timu yake iitwayo Miami FC ambayo inashiriki Ligi Daraja la Pili nchini Marekani.

Maldini anamiliki asilimia 50 ya hisa, huku sehemu iliyobaki ikiwa chini ya mfanyabiashara maarufu huko Italia, Riccardo Silva, ambaye ndiye rais wa klabu hiyo.

Hazard, Demba Ba (San Diego 1904)

Wakishirikiana na Yohan Cabaye na Moussa Sow, Eden Hazard na Demba Ba, ni wamiliki wa timu hiyo ya Ligi Daraja la Tatu huko Marekani. Tayari mastaa hao wamepanga kufanikisha ujenzi wa uwanja wa bei mbaya.

Katika mahojiano yake na vyombo mbalimbali vya habari, Demba Ba, amekuwa akisisitiza kuwa kumiliki timu ni ndoto yao ya muda mrefu.

Ronaldo De Lima (Real Valladolid)

Baada ya kuhaha kwa miaka minne, hatimaye Real Valladolid ilitinga La Liga msimu uliopita (2017-18). Septemba 3, mwaka huu, ndipo ilipotangazwa kuwa Ronaldo, mpachikaji mabao wa zamani wa Inter Milan na Real Madrid, amenuna sehemu kubwa ya hisa za klabu hiyo.

Kwa asilimia 51 ya hisa, Mbrazil huyo ndiye mwenye sauti ya mwisho katika maamuzi ndani ya timu hiyo inayoshika nafasi ya saba katika msimamo wa La Liga, ikiwa imejikusanyia pointi 12 katika michezo yake nane.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*