BASATA YAANDAA KONGAMANO KURUDISHA REGGAE

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Reggae Production House iliyo chini ya msanii mkongwe wa reggae, Innocent Nganyagwa, limeandaa kongamano maalumu kwa ajili ya kurudisha hadhi ya muziki wa reggae nchini itakayofanyika leo katika makao makuu ya Basata, Ilala jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo limepangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Basata uliopo Ilala Bungoni kuanzia saa nne asubuhi leo, ambapo litajadili mwelekeo wa muziki huo na kuja na mikakati bora ya kurudisha hadhi yake. Akizungumza na BINGWA, Ofisa habari wa Basata, Aristidesi Kwizela, alisema muziki huu umekuwa umeganda na kutokupiga hatua kubwa hali ambayo imewafanya wadau wa muziki kukosa burudani ambayo wamekuwa wakiipata huko nyuma kupitia kwa wasanii wakongwe kama Innocent Nganyagwa, Innocent Garinoma, Justine Kalikawa na wengineo.

“Nia ya Basata ni kuona wasanii na wadau wote wa muziki nchini wanahudhuria kongamano hili mahususi kwa lengo la kujadiliana kwa pamoja hatima ya muziki wa reggae, kupata historia ya jinsi ulivyokuwa huko nyuma, kutazama na kuburudika jukwaani na muziki wa mmoja wa wasanii wakongwe wa muziki huu,” alisema Alisema wanaamini kwamba, baada ya programu hii wasanii wa reggae na wadau kwa ujumla watakuwa na mwanzo mpya katika kurudisha hadhi ya muziki wa reggae nchini na kuhakikisha unaendelea kudumu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*