BARCA ILIVUTIWA NA VITU HIVI KWA YERRY MINA

CATALAN, Hispania

KLABU ya Barcelona mapema wiki hii ilitangaza kumsajili beki wa Colombia kwa kiasi cha euro milioni 12 kutoka katika klabu ya Palmeiras.

Baadhi ya wadau wa soka hawamtambui Mina, japo kuna wengine ambao wamebahatika kumtazama beki huyo wa kati kwenye timu yake ya taifa.

Tumekuandalia vitu vitano ambavyo viliivutia Barcelona hadi kupambana kuipigania saini ya Mina mwenye umri wa miaka 23.

 

  1. Uwezo wa kucheza mipira ya juu:

Urefu wake ni mita 1.93 na urefu wake ni silaha muhimu katika safu ya ulinzi sambamba na mashambulizi hasa mipira iliyokufa.

Mina ni mmoja wa mabeki waliofunga mabao mengi Amerika Kusini.

 

  1. Mwepesi kwenye matukio

Licha ya urefu wake, Mina ni beki ambaye miguu yake si mizito na mwenye maamuzi ya haraka hasa akiwa na mpira, na ndicho kinachotakiwa kwa mabeki wa Barcelona.

Ana kilo 75 lakini sio mzito kiasi hicho. Muda aliocheza soka Brazili katika klabu ya Palmeiras umemsaidia kuimarisha mbinu zake akiwa na mpira na hata kuendana na kasi ya mastraika wasumbufu waliopo kwenye Ligi Kuu nchini humo.

 

  1. Mbinu:

Muda wote anapokuwa na mpira huwa hakaribishi presha kwenye eneo lake na hutumia mbinu ya kuuondoa haraka, lakini kwa utulivu na hesabu nyingi, kwa hakika ni mchezaji halisi kabisa wa Barcelona.

 

  1. Kadi chache:

Kutokuwa mzito kwenye matukio kunamfanya Mina asiwe anacheza sana rafu na hivyo kupunguza uwezekano wa kunasa kadi nyingi iwe za njano au nyekundu.

Hadi sasa ana kadi moja tu nyekundu tangu aanze kucheza soka, aliyooneshwa mwaka 2013 dhidi ya Deportivo Pasto.

 

  1. Tegemeo:

Licha ya kwamba ndiyo kwanza ana miaka 23, Mina anatarajiwa kuanza moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Colombia kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Dunia, Barcelona ikaona isicheleweshe kumchukua mmoja wa wachezaji wanaotegemewa na taifa lake hasa ikizingatiwa hivi sasa anaonekana kuwa ni mchezaji anayekuja kwa kasi Colombia.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*