BARAKA THE PRINCE: NILIMFICHA MPENZI WANGU NAJ NILIPOBADILI DINI

CHRISTOPHER MSEKENA

WAKATI mwingine tena tunakutana hapa Jiachie na Staa Wako, safu inayokukutanisha na watu mbalimbali maarufu na unapata nafasi ya kuwauliza maswali, leo hii tupo na Baraka Adiero maarufu kama Baraka The Prince ambaye ni nyota wa Bongo Fleva anayefanya vizuri na wimbo Furaha.

SWALI: Sadick Mazoezi kutoka Kihonda Maghorofani, Morogoro, anauliza una elimu ya kiwango gani?

Baraka The Prince: Nina elimu ya cheti masuala ya uhandisi katika mawasiliano, shule ya msingi nilisoma Pamba na sekondari ya Tabasamu pale Mwanza na baada ya hapo nikajiunga na Chuo cha Mtakatifu Joseph, lakini pia nina mpango wa kurudi tena shule Mungu akijaalia.

SWALI: Narro Kambona wa Mwananyamala Kisiwani, anauliza sababu gani zilifanya uondoke Rockstar na uhusiano wako na Ali Kiba upo vipi?

Baraka The Prince: Kuna vitu ambavyo nafikiri havikwenda sawa mimi na Rockstar japo si vizuri kuviweka wazi kwa sababu ni mambo ya kikazi, sina tatizo naye japokuwa sijawahi kuonana naye tangu nimetoka Rockstar.

SWALI: Mpole Classic kutoka Kijichi anauliza, ni kweli mlitengana na mpenzi wako Naj?

Baraka The Prince: Hatukuachana, tulipeana likizo kidogo na sasa hivi tupo pamoja kwa sababu naona kabisa anastahili kuwa mke wangu.

SWALI: Ally Ally wa Nakapanya Tunduru, anauliza sasa hivi unasimamiwa na nani na uhusiano wako na mabosi zako wa zamani upo vipi?

Baraka The Prince: Sasa hivi najisimamia mwenyewe kwenye lebo yangu ya Bana Music Lab ambayo inasimamia muziki wa Naj pia. Nashukuru nipo vizuri na viongozi wangu waliopita kama Kidboy, Mgalula, Seven Mosha niliwahi kuwaomba msamaha.

SWALI:  Ezra Suleiman anauliza, umewahi kuimba wimbo unaohusu maisha yako halisi?

Baraka The Prince: Inatokea mfano ni wimbo wangu unaoitwa Sina, nilipata wazo la kuimba baada ya siku niliamka nikajikuta sina chochote, sina pesa, gari haina mafuta, king’amuzi kimekata halafu kama unakumbuka mwaka jana sikufanya shoo yoyote kwa hiyo sikuwa na pesa.

SWALI: Michael Ndondole wa Mufindi, Iringa, anauliza kwanini hutoi nyimbo mfululizo kama wasanii wengine?

Baraka The Prince: Kila msanii ana mipango yake, kuna mipango yangu ilikuwa haijakaa sawa ila sasa hivi mashabiki zangu watarajie ngoma kwa ngoma.

SWALI: Sam Classic wa Bungulo anauliza, ni kweli umebadili dini na sababu zipi zilifanya ufanye maamuzi hayo?

Baraka The Prince: Ni kweli nimebadili na jina la Kiislamu naitwa Abdumalik na nilifanya kwa maamuzi yangu kwa sababu mimi si wa kwanza kuna ndugu zangu ambao nao walibadili dini na Naj mwenyewe alikuwa hajui kama nimebadili dini mpaka alivyoona mtandaoni, nilimficha sikutaka ajue.

SWALI: Twalib Toshi wa Msata Chalinze anauliza, kwanini wasanii wa sasa hivi hamtoi albamu?

Baraka The Prince: Siwezi kuwajibia wengine ila kwangu tayari nimetoa EP albamu yangu inaitwa African Prince, ipo mtandaoni ina ngoma kama Sina, Tokota, Maya, Unanigasi, Rhumba, Furaha na Mawazo, Twalib fanya uitafute kaka.

Wiki ijayo tutakuwa na Wakazi au Shilole, tuma swali lako kwao kupitia namba hapo juu, meseji tu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*