Bao lampa Tshishimbi matumaini kubaki Yanga

NA MWAMVITA MTANDA

KIUNGO wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi, amesema baada ya kufunga bao la kusawazisha dhidi ya KMC, amepata matumaini ya kuendelea kubaki ndani ya kikosi hicho.

Yanga walifanikiwa kuitandika KMC mabao 2-1, katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tangu kuanza kwa ligi hiyo msimu huu, Tshishimbi, hajafanikiwa kufunga huku akiwaacha mashabiki wa timu hiyo wakilalamika kuwa ameshuka kiwango.

Akizungumza na BINGWA jana, Tshishimbi, alisema anatambua uwezo wake katika soka, lakini kuna wakati mambo yanakuwa magumu anapokuwa uwanjani.

“Siku hazifanani, halafu haiwezekani kila mmoja afunge japo kuna wakati ambao ni lazima kufunga kulingana na nafasi zao, lakini nashukuru Mungu najiona sasa nipo fiti zaidi.

“Pia itanisaidia na kulinda kibarua changu, kwani nipo hapa kwa ajili ya kusaidia timu yangu kufanya vizuri, sasa ikiwa navurunda ni rahisi kupoteza  matumaini kwa mabosi wangu,” aliongeza Tshishimbi.

Aidha, Tshishimbi, alisema kiwango cha mchezaji hakiwezi kusimama wakati wote, kuna muda anaweza kufanya vibaya endapo kama kuna jambo linamtatiza.

Mkongo huyo alieleza kuwa bado ana kiu kubwa ya kuendelea kucheza soka, hivyo ataendelea kufanya juhudi ili kurudi katika hali yake ya zamani.

Inadaiwa kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wanasadikika kuondoka ndani ya timu hiyo baada ya kumaliza msimu naye ni miongoni mwao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*