googleAds

BAO LA AJIB GUMZO TAIFA YANGA WAZIDI KUNOGA TAIFA

NA WINFRIDA MTOI

Ibrahim  Ajib amefunga bao moja na kutengeneza jingine Yanga ikiifunga Mbao FC 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa jana Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ajib ambaye ameachwa katika kikosi cha Taifa Stars kinachoondoka kesho kwenda kuikabili Cape Verde katika mchezo wa kufuzu Kombe la Afrika 2019, alifunga bao la pili kwa staili ya aina yake.

Akiwa katika boxi la penalti dakika za majeruhi kipindi cha pili, Ajib alipiga ‘tikitaka’ baada ya mabeki wa Mbao FC kushindwa kuokoa shambulizi lililofanywa na Yanga.

Awali katika dakika ya 16, Ajib aliuchonga kwa ufundi mpira wa adhabu ambao uliungwanishwa kwa kichwa na kiungo Raphael Daudi.

Adhabu hiyo iliyotolewa na mwamuzi Hence Mabena kutoka Tanga ilitokana na mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo, kufanyiwa madhambi na beki wa Mbao FC, Amos Charles.

Mbao FC walianza mchezo wa jana kwa kasi na dakika ya nane, mshambuliaji Said Hamis alipiga shuti lakini mpira ukatoka.

Yanga walipata nafasi nzuri kuongeza bao la pili dakika ya 21 baada ya Makambo kuwahadaa mabeki wa Mbao FC na kufumua shuti lililogonga mwamba kabla ya kipa Hashim Mussa kuudaka.

Dakika moja baadaye, Mbao FC walilisakama lango la Yanga ambapo kipa Benno Kakolanya alilazimika kupangua mara mbili shuti la Abubakary Ngalema na Pastory Antanas.

Katika dakika ya 27, Mbao FC walipata kona ambayo Hamis alimuanzishia Ngalema aliyepiga shuti likagonga mwamba na kutoka nje.

Mwamuzi Mabena alimuonywa kwa kadi ya njano Hamidu Abdulkarimu wa Mbao FC baada ya kumfanyia madhambi Paul Godfrey.

Katika dakika ya 40, mchezo ulilazimika kusimama kupisha kipa wa Yanga, Kakolanya, kupata matibabu baada ya kuonekana akishika paja la mguu wake wa kushoto.

Zikiwa zimebaki dakika mbili kipindi cha kwanza kumalizika, Makambo alimtengea pasi nzuri Mateo Anthony lakini shuti lake likadakwa na kipa Mussa.

Yanga walipata pigo dakika ya 56 baada ya kipa Kakolanya kushindwa kuendelea na mchezo kutokana na kubanwa na msuli na nafasi yake kuchukuliwa na Klaus Kindoki.

Kakolanya amekuwa katika kiwango kizuri hadi kuitwa Taifa Stars lakini sasa inasubiriwa ripoti ya daktari kuona kama atakuwa kwenye msafara utakaoenda Cape Verde.

Mbao FC nusura wapate bao dakika ya 72 lakini shuti lililopigwa na Hussein Selemani lilikwenda pembeni.

Kwa matokeo hayo, Yanga ambayo haijapoteza mchezo inajikusanyia pointi 16 sawa na Singida United lakini wanawazidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Timu inayoongoza ligi ni Mtibwa Sugar ikiwa na pointi 17.

Yanga: Beno Kakolanya/Klaus Kindoki, Paulo Godfrey, Gadiel Michael,  Andrew Vincent, Kelvin Yondan, Feisal Salum, Deus Kaseka, Raphael Daudi, Heritier Makambo, Ibrahim Ajib na Anthony Mateo/Thaban Kamusoko.

Mbao: Hashim Mussa, Vincent Philipo, Amos Charles, David Mwasa, Peter Mwangosi, Ally Mussa, Emmanuel Mtumbuka, Hussein Seleiman, Said Khamis, Pastory Antanas na Abubakary Ngalema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*